Na Atley Kuni, WAF-Dar es salaam
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea kuimarisha utayari wa jamii kukabiliana na majanga kwa kuwajengea uwezo watendaji ngazi ya Mtaa pamoja na viongozi wa jamii, ili waweze kuchukua hatua za awali pindi majanga yanapotokea.
Hali hii imebainishwa Oktoba 3, 2026 na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dkt. Peter Nsanya wakati wa mapitio na utayari wa timu ya Uharaka ya mawasiliano ya Ushirikishwaji wa jamii kwa lengo ni kuhakikisha jamii inakuwa sehemu ya maandalizi na mwitikio wa majanga hususan ni Elinino na Ebolla.
Dkt. Nsanya amesema, Halmashauri imekuwa ikiwashirikisha wataalam wa hali ya hewa kutoa elimu kwa wananchi, huku pia watu maarufu na viongozi wa jamii wakipewa taarifa sahihi ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Aidha, viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa wakitembelea maeneo yaliobainishwa kuwa na uwezekano wa kukumbwa na majanga.
“Halmashauri inatumia viongozi wa Mitaa ambao wanafahamu vizuri mahitaji na changamoto za wananchi katika maeneo yetu. Pia, kila Kata imeainisha maeneo yenye viwango vya juu vya hatari, ambapo Halmashauri imshirikiana na viongozi wa maeneo hayo pamoja na TARURA kupanga hatua stahiki za kuzuia na kukabiliana na athari hizo zinazoweza kutokea” amesema Dkt. Nsanya,
Dkt. Nsanya ametolea mfano eneo la Tandale ambako hatua zilizochukuliwa ikiwemo ujenzi wa Mto Ng’ombe zimechangia kuongeza utayari wa jamii huku Halmashauri ikiwaimefanya zoezi la mapping na kubainisha maeneo manane pamoja na sub-zones, hatua inayosaidia kutambua kwa haraka maeneo yanayohitaji mwitikio wakati wa dharura.
Akiongelea juu ya mfumo wa taarifa, Dkt. Nsanya amefafanua kuwa, Halmashauri hutumia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (CHWs), wenyeviti wa Mitaa na viongozi wengine kama vyanzo muhimu vya taarifa kutoka kwa wananchi hali iliyosaidia pia wakati wa COVID-19, ambapo taarifa za watu waliokuwa hawajaonekana katika jamii kwa muda ziliwasilishwa kwa wataalamu wa afya kwa ajili ya ufuatiliaji.
Amesema Halmashauri pia imeendelea kuweka njia za mawasiliano kwa wananchi, zikiwemo namba za simu za viongozi wa Wilaya na mfumo wa e-Mrejesho, unaowawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko na mrejesho kwa Afisa Malalamiko, lakini pia inaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa elimu ya afya na tahadhari kwa jamii hatua ambayo imeongeza uelewa kwa jamii.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, UNICEF na mdau TIP inaendelea na zoezi kupitia na kufanya maboresho ya nguzo ya usimamizi wa masuala Elinino na Ebolla kwa mikoa 12 nchini inayotajwa kuwa kwenye tahadhari ya juu ya majanga hayo.

