Msimu wa mvua unapokaribia maandalizi ya mapema si jambo la hiari, bali ni hatua muhimu ya kulinda miundombinu ya barabara, usalama wa watumiaji na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya barabara.
Katika kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha mtandao wa barabara za mijini na vijijini unapitika kwa usalama na wakati wote, Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa, ikiwemo mvua ya El NiƱo kama iliyotolewa taarifa na Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA).
Katika muktadha huo, Mtendaji Mkuu wa TARURA ametoa wito kwa Mameneja wa Mikoa na wilaya kuhakikisha usafi na uondoaji wa uchafu katika mitaro, makaravati na maeneo yote muhimu ya kupitisha maji unafanyika kwa wakati kabla ya mvua kubwa kuanza.
Wito huu una maana pana zaidi ya kusafisha miundombinu. Ni sehemu ya mkakati wa kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Mitaro na makaravati ni sehemu muhimu ya mfumo wa ulinzi wa barabara zinapokuwa zimejaa taka, mchanga, majani au kuzibwa kwa namna yoyote, uwezo wa maji kupita hupungua na hatimaye maji huweza kuingia kwenye eneo la barabara. Hali hiyo inaweza kusababisha mmomonyoko wa kingo, kuharibika kwa tabaka la barabara, kutengeneza mashimo, kuathiri madaraja na makaravati na wakati mwingine kusababisha barabara kukatika.
Kwa hiyo,usafi wa mitaro na makaravati ni sehemu ya matengenezo ya barabara na si kazi ya msimu wa mvua pekee.
TARURA ina wajibu wa kuhakikisha miundombinu hii inakuwa katika hali inayowezesha maji kupita kwa ufanisi. Hata hivyo, mafanikio ya jitihada hizi yanahitaji ushirikiano wa wananchi. Utupaji wa taka kwenye mitaro, ujenzi unaoziba njia za maji na shughuli nyingine zinazozuia mtiririko wa maji vinaweza kuongeza ukubwa wa tatizo.
Ni muhimu wananchi kutambua kuwa kulinda miundombinu ya barabara ni jukumu la pamoja.
Katika kipindi hiki, Mameneja wa Mikoa na Wilaya wanapaswa kuendelea na ukaguzi wa barabara, mitaro, makaravati, madaraja na maeneo yenye historia ya kuathiriwa na maji huku hatua za matengenezo zikichukuliwa mapema.
Aidha, maeneo hatarishi yanapaswa kutambuliwa na kuwekwa katika mpango wa ufuatiliaji wa karibu wakati wa mvua.
Tunawasihi wananchi kushirikiana na TARURA kwa kutoa taarifa mapema kuhusu mitaro iliyozibwa, makaravati yaliyoharibika, maeneo yenye maji mengi na sehemu za barabara zilizo katika hatari ya kuathirika. Taarifa hizi zitasaidia hatua kuchukuliwa kwa wakati.
Pia, watumiaji wa barabara wanakumbushwa kuchukua tahadhari wakati wa mvua hasa katika maeneo yenye maji mengi, madaraja na makaravati na kufuata maelekezo ya wataalamu na mamlaka husika.
TARURA inaendelea kuimarisha miundombinu, wananchi nao walinde miundombinu hiyo.
