Na Jeremia Mwakyoma

GEITA – OKTOBA 1, 2026

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetunukiwa Tuzo maalumu na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa lengo la kutambua mchango na ushiriki wake katika Jukwaa la Fursa za Kiuchumi linalofanyika Sambamba na Maonesho ya tisa ya Kitaifa ya Teknolojia za Madini Mkoani Geita.

Akiongea wakati wa kukabidhi Tuzo hiyo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TSN Ndg. Patrice Simbachawene amesema kuwa Jukwaa la Fungua Fursa pamoja na kuangazia shughuli za uchimbaji madini na mnyororo wake wa biashara katika Mkoa wa Geita, linatambua mahitaji makubwa ya huduma za Afya za kibingwa kwa.wadau walio katika sekta ya madini.

“Nitumie fursa hii kuishukuru BMH kwa kushiriki katika Jukwaa la Fungua Fursa na Maonesho ya Teknolojia za Madini kwa kuleta huduma za kibobezi za matibabu na kuzitoa hapahapa katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, wadau wa sekta ya madini na Wananchi wa Geita na mikoa ya jirani watapata huduma za kibingwa kwa muda wote hadi maonesho yanapokamilika Oktoba 3, 2026” alisisitiza Ndg. Simbachawene.

Akishukuru kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Mugisha Nkoronko akiwa na Jopo la Mabingwa kutoka BMH amesema kuwa BMH ni mshirika wa kimkakati kwenye Jukwaa la Fungua Fursa na Wadau wote wa Sekta ya madini, imeweka kipaumbele cha Afya zao na maisha yao kwa ujumla kwa kuwahakikishia huduma bora, za ubobezi, salama na zinazopatikana kwa wakati muafaka.

“BMH ipo Dodoma lakini inawafikia watu mbalimbali na mikoa mbalimbali ikiwemo Geita, hivyo natoa Rai kwa wananchi wote na wadau wa sekta ya madini mikoa yote kanda ya ziwa kufika BMH kupata huduma za kibobezi ili wananchi wawe na Afya bora iwasaidie katika shughuli zao za uzalishaji” alisistiza Dkt. Nkoronko.