Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kusimamia kuunganishwa kwa mifuko na programu 75 za uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwa mfuko mmoja. Amesema mfuko huo unapaswa kurahisisha upatikanaji wa mitaji na dhamana, hasa kwa vijana ambao hawakidhi masharti ya kukopa katika taasisi za fedha.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo alipokagua maonesho ya vijana, kabla ya kushiriki Hafla ya kitaifa ya kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili katika sekta ya Maendeleo ya Vijana, iliyofanyika Ukumbi wa Super Dome Masaki.

Akihutubia katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema, shilingi bilioni 200 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana zitolewe bila upendeleo na ziwafikie vijana wa mijini na vijijini, wakiwemo wenye ulemavu.

Makamu wa Rais, ameonya matumizi ya fedha hizo katika kulipa posho za watumishi au kununua magari. Amesema mafanikio ya mpango huo yapimwe kwa kuangalia biashara zilizoanzishwa, zilizokua na ajira zilizozalishwa.

Pia ametoa rai kwa Wizara, Taasisi za Umma na Halmashauri kuwalipa kwa wakati vijana wanaotekeleza zabuni ili ucheleweshaji wa malipo usikwamishe biashara zao.

Akieleza ukubwa wa changamoto ya ajira, Ndejembi alisema takribani vijana 900,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka na karibu mmoja kati ya kumi hupata ajira rasmi. Alisema taasisi za umma zimeahidi kutoa takribani nafasi 600 za mafunzo kwa vitendo, zitakazotangazwa hivi karibuni taratibu za uratibu zitakapokamilika. Nafasi hizo ni hatua ya awali kuelekea lengo la kupata angalau nafasi 10,000 katika mashirika ya umma na 20,000 katika sekta binafsi.

Makamu wa Rais ametoa wito wa Mashindano ya Afcon 2027 kutumika kama fursa kwa vijana, kupitia uwezeshaji wa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kuhudumia wageni na kufanya shughuli mbalimbali katika mashindano hayo. Amesema ni heshima kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo katika miji mitatu ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar, hali itakayopelekea fursa ya ajira kwa vijana, ongezeko la vipato na ongezeko la stadi za maisha za kudumu.

Makamu wa Rais ameipongeza Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa kazi ya kuwafikia vijana na kuwataka Vijana wasikate tamaa kutokana na changamoto za ajira na ukosefu wa mitaji.

Amewahimiza Vijana kuendelea kujifunza, kubuni na kutumia fursa zinazojitokeza. “Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko jikoni, anawaandalia mambo mazuri zaidi,” alisema, akiwataka vijana kukaa “mkao wa kula,” kujiandaa kutumia fursa na kuwasilisha mawazo yao kupitia ofisi hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka, alisema takribani shilingi bilioni 52.69, sawa na asilimia 26 ya fedha za mpango wa shilingi bilioni 200, zilikuwa zimepelekwa kwa wizara zinazoutekeleza.

Kwa mujibu wa Waziri Nanauka, mpango huo na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa pamoja vimechangia kuzalisha takribani ajira 44,615 kupitia miradi 3,950 katika mwaka wa fedha unaoendelea. Alisema mikopo inayotolewa kupitia ofisi hiyo haina riba na muda wa kuanza marejesho huzingatia mzunguko wa uzalishaji.

Nanauka ametoa mfano wa Imani Mpinga, mkulima wa alizeti aliyepata shilingi milioni 263 kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta ya alizeti katika kijiji cha Makunda, ambaye tayari ameanza kuuza mafuta hayo.

Kuhusu manunuzi ya umma, Nanauka amesema vikundi vya vijana vimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12.99, huku lengo likiwa kufikia shilingi bilioni 50 kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha. Alisema pia takribani vijana 400,000 wamejisajili katika mfumo wa Youth Empowerment System (YES), unaowapa taarifa kuhusu fursa za ajira na uwezeshaji.

Akiwasilisha salamu za Umoja wa Wabunge Vijana kwa niaba ya mwenyekiti wake, Zainab Katimba, Mbunge wa Malindi Muhsin Haji Ussi amesema vijana wanataka kuona ahadi zikitekelezwa na kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao. Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa ofisi yenye dhamana mahsusi ya maendeleo ya vijana kumeimarisha uratibu wa ajenda inayohusisha Wizara na Taasisi nyingi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Dkt. Regina Christopher Malima, akiwasilisha salamu za Bunge, ametoa rai ya uratibu wa mipango na bajeti za vijana uimarishwe katika wizara, taasisi na halmashauri. Alisema Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana inahitaji taarifa za utekelezaji kutoka sekta mbalimbali ili kufuatilia matumizi ya fedha, maeneo yaliyofikiwa na matokeo yaliyopatikana.

Hafla hiyo iliyofanyika chini ya kaulimbiu “Mwaka Mmoja, Vijana Pamoja.” imewakutanisha vijana, viongozi wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Taasisi za fedha na wadau wa sekta binafsi.