Na MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, amewataka wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu kuzingatia uzalendo na uadilifu katika kutumia taaluma zao, akisema elimu bila uaminifu kwa nchi inaweza kuchangia matatizo katika jamii.
Amesema wahitimu wanapaswa kutumia elimu waliyoipata kujenga na kulitumikia taifa badala ya kujihusisha na migogoro isiyo na tija, akisisitiza kuwa uzalendo ni msingi muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wasira alitoa kauli hiyo aliposhiriki mahafali leo Novemba 23, 2026 katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya Karume Zanzibar , ambapo alisema taaluma mbalimbali walizonazo wahitimu, zikiwemo uhasibu na sayansi ya jinsia, zinapaswa kuwa chachu ya kulitumikia taifa kwa uaminifu.
Alisema changamoto inayojitokeza ni baadhi ya watu wanapohitimu kushindwa kuelekeza nguvu zao katika kutumia elimu kutatua changamoto za nchi na badala yake kujiingiza katika migogoro isiyokuwa na manufaa.
“Nyinyi mnayo taaluma, mmesoma, wengine ni wahasibu, wengine mmesoma sayansi ya jinsia na kadhalika. Yote hayo yanaweza kuwasaidia, lakini uzalendo ni kitu muhimu sana. Lazima mhakikishe mnakuwa watu mnaotumikia nchi yenu kwa uaminifu kweli,” alisema Wassira.
Pia alisisitiza kuwa migogoro haiwezi kuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili Watanzania, bali kinachohitajika ni kukaa chini, kufikiri na kutafuta njia za kutumia elimu na maarifa kuleta maendeleo.
Wasira alieleza kuwa kongamano lililofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, jijini Dar es Salaam, linatoa fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa dhamira ya kuwawezesha vijana kujiajiri.

