Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

TANZANIA imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, huku vifo vitokanavyo na uzazi vikishuka kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kuongoza Afrika katika sekta hiyo.

Hayo yamesemwa leo Novemba 23,2026 jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Makuwani, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa Serikali katika kuboresha miundombinu, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya.

Amesema mikataba ya uwajibikaji iliyosainiwa na wakuu wa mikoa kupitia kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama mwaka 2018 na mkataba wa kuimarisha lishe mwaka 2022 imekuwa chachu ya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto nchini.

Amesema bajeti ya sekta ya afya imeongezeka kutoka Sh trilioni 2.46 mwaka 2023/24 hadi Sh trilioni 3.7 kwa mwaka wa fedha 2026/27, huku upatikanaji wa dawa za afya ya uzazi, mama na mtoto ukifikia zaidi ya asilimia 85.

Ameongeza kuwa zahanati zimeongezeka kutoka 4,127 hadi 6,589, vituo vya afya kutoka 535 hadi 1,067 na hospitali za wilaya kutoka 77 hadi 194, huku magari ya kubebea wagonjwa yakiongezeka kutoka 540 mwaka 2021 hadi 1,113 mwaka huu.

Dkt. Makuwani amesema pia vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 36 kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000, huku mfumo wa rufaa wa kielektroniki wa m-Mama ukiwezesha kusafirisha wagonjwa 250,000 hadi Agosti 2026.

Aidha amesema mafanikio hayo yamechangia Rais Samia Suluhu Hassan kutunukiwa tuzo ya Goalkeepers ya Gates Foundation Februari 2025 na kutambuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika huduma za afya ya mama na mtoto.

Amesema mkutano wa tatu wa afya ya uzazi, mama na mtoto na lishe utafanyika Novemba 25 hadi 27 mwaka huu, ukiwa na lengo la kuweka mikakati ya kufikia malengo ya mwaka 2030, ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi hadi chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000.

Amesema Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa mkutano huo, ambapo atazindua ripoti ya hali ya vifo vya uzazi na watoto, kusaini mkataba wa pili wa uwajibikaji na kuwakabidhi wakuu wa mikoa mpango wa nne wa huduma za afy tiqa ya uzazi na mtoto.