Na.Sophia Kingimali.
WASANII na wadau wa muziki na sanaa nchini wanatarajia kuandaa hafla maalumu ya kumuenzi Meneja wa wasanii, Said Fella, kwa kutambua mchango wake katika kukuza na kuendeleza tasnia ya muziki nchini.
Tukio hilo litakalojulikana kama “A Celebration of Legacy”, linatarajiwa kufanyika Jumapili, Novemba 29, 2026, kupitia hafla ya uzinduzi wa Gala itakayowakutanisha wadau mbalimbali wa muziki na sanaa.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya tukio hilo,Mwenyekiti wa Jumuiya ya mitandao ya kijamii nchini (JUMIKITA) Shabani Matwebe amesema lengo ni kutoa heshima kwa Said Fella kutokana na mchango wake katika safari ya maendeleo ya muziki wa Tanzania.
Amesema hafla hiyo itakuwa fursa kwa wasanii na wadau wa sanaa kukutana na kusherehekea mafanikio yaliyopatikana katika tasnia hiyo kupitia mchango wa Fella.
Aidha, tukio hilo linatarajiwa kutoa nafasi kwa wadau kutambua historia ya Said Fella na mchango wake katika kukuza muziki wa Tanzania, huku likisisitiza umuhimu wa kuthamini watu waliochangia maendeleo ya sekta hiyo.
Kaulimbiu ya tukio hilo ni Heshima kwa Mkubwa Fella, ikiwa ni sehemu ya kuenzi urithi wake na kuhamasisha utamaduni wa kuthamini mchango wa watu walioleta mabadiliko katika tasnia ya sanaa nchini.

