NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
SIMBA Queens imefuzu kucheza fainali ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake baada ya kuichapa Yanga Princess mabao 3-0 katika nusu fainali ya pili iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeiwezesha Simba Queens kutinga fainali, ambapo itakutana na JKT Queens Oktoba 3, 2026, katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Mchezo huo ulianza kwa kasi na ushindani mkubwa, huku Simba Queens ikitawala baadhi ya vipindi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga.
Mashambulizi ya Simba yalizaa matunda dakika ya 23, baada ya Vivian Corazone kuifungia timu hiyo bao la kwanza na kuiweka mbele kwa 1-0 hadi mapumziko.
Yanga Princess ilipata pigo dakika ya 36, baada ya Ritticia Nabbosa kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea madhambi Mary Siyame wa Simba Queens, hivyo kuifanya Yanga kucheza pungufu kwa sehemu kubwa ya mchezo.
Simba Queens iliendelea kucheza kasi katika kipindi cha pili na hatimaye kufanikiwa kuongeza mabao mawili na kukamilisha ushindi wa 3-0.
Fainali hiyo itakuwa marudiano ya fainali ya mwaka 2025, ambapo JKT Queens iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba Queens na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo.
Timu hizo pia zilikutana katika fainali ya mwaka 2023, ambapo Simba Queens ilitwaa taji baada ya sare ya 1-1 na kisha kushinda kwa penalti.
Hivyo, mchezo wa Oktoba 3 utakuwa na historia yake, huku Simba Queens ikilenga kurejesha taji hilo na JKT Queens ikisaka kuendeleza ubabe wake baada ya kuibuka mshindi katika fainali iliyopita.
