Taifa Stars imeendelea na safari yake ya kuwania nafasi katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Madagascar, katika mchezo wa Kundi L uliochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa d’Honneur, Meknes nchini Morocco.

Matokeo hayo yameifanya Tanzania kuwa pointi moja kwenye msimamo wa kundi hilo, baada ya kuanza kampeni kwa kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau katika mchezo wa kwanza.

Stars ilipata bao lake kupitia Cyprian Kachwele dakika ya 39, akimalizia pasi ya Feisal Salum na kuiwezesha Tanzania kwenda mapumziko ikiwa na faida ya bao moja.

Hata hivyo, Madagascar ilirejea kipindi cha pili ikiwa na msukumo mkubwa na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 50 kupitia Nicolas Fontaine, hali iliyofanya timu hizo kugawana pointi.

Kocha Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa katika kipindi cha pili, akiwamo Haji Mnoga aliyeingia kuchukua nafasi ya Miano van den Bos aliyeumia. Simon Msuva na Charles M’Mombwa pia waliingia kuchukua nafasi za Kachwele na Feisal Salum.

Pamoja na mabadiliko hayo, Stars haikufanikiwa kupata bao la pili na hivyo kulazimika kuridhika na sare..

Fainali hizo zinatarajiwa kuwa na umuhimu wa kipekee kwa Tanzania, Kenya na Uganda ambao kwa pamoja watakuwa wenyeji wa michuano hiyo.

Hata hivyo licha ya mtaifa haya matatu kushiriki katika kuwania nafasi, tayari wamepewa tiketi kutokana kuwa wenyeji wa michuano hiyo.