Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea na kukagua Mradi wa Mji wa Michezo Zanzibar (AFCON), na kujionea hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayotekelezwa katika eneo hilo.
Rais Dkt. Mwinyi amefanya ziara hiyo leo, tarehe 28 Septemba 2026, Fumba, Wilaya ya Magharibi “B”, Unguja, ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kawaida kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Katika ziara hiyo, amekagua miundombinu ya michezo ikiwemo uwanja wa mazoezi, uwanja wa mpira wa miguu, bwawa la kuogelea lenye urefu wa mita 50 pamoja na bwawa maalum kwa mchezo wa kuruka majini (Diving Pool).
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametembelea eneo la wazi la Fan Zone lenye uwezo wa kuhudumia watu 4,000, pamoja na miundombinu ya bandari inayojengwa kwa ajili ya boti ndogo na kubwa.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba 2026, hatua itakayoiwezesha Zanzibar kuwa miongoni mwa wenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

