Ukurasa mpya wa kimkakati na wa kihistoria umefunguliwa rasmi katika uhusiano wa diplomasia na uchumi kati ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania na Usultani wa Oman, kufuatia kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Uwili Kati ya Nchi hizo tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Mashauriano ya Kisiasa mwaka 2009.

Mkutano huo uliofanyika Septemba 28, 2026 jijini Muscat, Oman ambao umeongozwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya nje wa Oman Mhe. Sheikh Khalifa Al-Harthy, pande hizo mbili zimekubaliana kuimarisha uhusiano wao wa kihistoria; kidugu na kirafiki kwa kutumia nafasi ya kijiografia ya nchi hizo kuwa madaraja na vituo muhimu vya biashara na uwekezaji kati ya Afrika na Ghuba. 

Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb.) amebainisha kuwa mkutano huo ni hatua kubwa ya kimfumo inayolenga kubadilisha nia njema kuwa matokeo yanayoonekana.  

Mhe. Londo ameishukuru Oman kwa kuendelea kuwekeza Tanzania Katika Sekta mbalimbali huku akiwakaribisha wawekezaji kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Oman (OIA) kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji, gesi asilia, na madini. OIA imeonesha nia ya kuwekeza nchini kupitia ubia wa kibiashara na miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Kupitia mkutano huo Tanzania na Oman zimejadiliana kwa kina kuhusu umuhimu wa kuimarisha ziara za viongozi na wataalamu katika ngazi mbalimbali, kwa lengo la kuongeza fursa za kubadilishana uzoefu, maarifa na utaalamu, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa makubaliano baina ya nchi hizo.

Aidha, wamejadili Ushirikiano Katika Sekta Muhimu na za Kimkakati ikiwemo Biashara na Uwekezaji, kilimo, afya, elimu, Uchumi wa buluu na Fursa za Kazi na ajira rasmi pamoja na utalii na malikale ambazo zitasaidia kutekeleza kwa ufanisi Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Dira ya Maendeleo Oman 2040.

Mkutano huo unaiweka diplomasia ya nchi hizo mbili kwenye mwelekeo mpya unaotoka kwenye utamaduni na undugu wa kale, na sasa kujikita kwenye ushirikiano thabiti wa biashara, uwekezaji wa kimkakati, na fursa za kiuchumi zitakazonufaisha wananchi wa mataifa hayo mawili.