NA DENIS MLOWE, IRINGA

KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini, Arnold Mvamba, kwa niaba ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Alifu Abri, amekabidhi msaada wa kompyuta moja pamoja na mabati 30 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya kuishi wahudumu wa afya katika Zahanati ya Kijiji cha Usolanga, Kata ya Malengamakali, Wilaya ya Iringa Vijijini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mvamba amesema msaada huo umetokana na ahadi iliyotolewa na Alifu Abri wakati wa ziara yake katika eneo hilo, ambapo wananchi walieleza changamoto ya ujenzi wa nyumba ya watumishi wa afya pamoja na uhitaji wa vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kusaidia shughuli za utoaji huduma katika zahanati hiyo.

Amesema awali walipofika Usolanga walifanya mazungumzo na wananchi na kubaini kuwa jengo la nyumba ya mtumishi lilikuwa limefikia hatua ya kuezekwa, hivyo Abri akaahidi kuchangia mabati ili kusaidia kukamilisha sehemu hiyo ya ujenzi.

“Nilipofika hapa pamoja na ndugu yetu Alifu Abri, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, aliahidi kutoa mabati 29, nami nikaahidi kuchangia bati moja. Hivyo jumla yake ni mabati 30,” amesema Mvamba.

Amesema utekelezaji wa ahadi hiyo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano kati ya viongozi, wananchi na Serikali katika kuchochea maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Mvamba amesema licha ya idadi ya mabati hayo kuonekana kuwa ndogo kwa baadhi ya watu, hatua hiyo ina umuhimu mkubwa kwa sababu inaonesha namna wadau mbalimbali wanavyoweza kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Ameongeza kuwa pamoja na mabati hayo, Alifu Abri ametoa kompyuta moja kwa ajili ya kusaidia shughuli za wahudumu wa afya katika zahanati hiyo, hatua ambayo amesema itasaidia kuboresha utendaji wa huduma.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Malengamakali, Stephano Msisi, amesema maendeleo katika kata hiyo yanahitaji ushirikiano wa Serikali, viongozi, wananchi, taasisi mbalimbali pamoja na wadau binafsi na kimshukuru Alifu Abri kwa kuwa kiongozi wa mfano katika kusaidia jamii ya Usolanga mara kwa mara.

Msisi amesema baada ya wananchi kueleza changamoto zao, walimfikishia Alifu Abri ombi la kusaidia ujenzi wa nyumba ya watumishi wa afya pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kielektroniki kwa ajili ya zahanati hiyo.

Amesema Abri alikubali kusaidia na hatimaye ametimiza ahadi yake kwa kukabidhi mabati pamoja na kompyuta, jambo ambalo amesema limeongeza nguvu katika juhudi za wananchi kukamilisha jengo hilo.

“Kwa moyo wa huruma na upendo, wa Alifu Abri aliaidi mabati na kompyuta. Leo tunatoa taarifa kwenu kwamba ahadi hiyo imetekelezwa,” amesema Msisi.

Amesema nyumba hiyo itakapokamilika itakuwa muhimu kwa watumishi wa afya watakaokuwa wakihudumu katika zahanati hiyo, hivyo kusaidia upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa Usolanga na maeneo jirani.

Amesema msaada huo haupaswi kuonekana kama mali ya mtu binafsi, bali ni mchango kwa wananchi na jamii kwa ujumla, hivyo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana katika kukamilisha ujenzi huo.

Msisi ametoa shukrani kwa Alifu Abri kwa kutambua changamoto ya wananchi wa Usolanga na kuitikia ombi lao, huku akisema bado kuna mahitaji mbalimbali yanayohitaji ushirikiano wa viongozi, wananchi na wadau wengine.

Amesema wananchi wa Kata ya Malengamakali wanaendelea kutambua mchango wa viongozi na wadau wanaowasaidia katika shughuli za maendeleo, akisisitiza kuwa nguvu ya wananchi na ushirikiano ndio msingi wa kukamilisha miradi mbalimbali.

Makabidhiano hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za kijamii, hususan afya, katika maeneo ya vijijini.