NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, wametuma salamu za pole na rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi kufuatia kifo cha Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Mama Fatma Karume amefariki dunia usiku wa Septemba 21, 2026 ambapo katika salamu zake, Dk. Mwinyi alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo hicho, akieleza kuwa msiba huo ni pigo kwa familia na Taifa kwa ujumla.

Amesema kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, familia yake na wananchi anatoa pole kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, familia ya Hayati Sheikh Karume, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.

Amesema Taifa litamkumbuka Mama Fatma kwa heshima aliuoipatia Zanzibar na watu wake na kwamba serikali inathamini mchango wake katika jamii na historia ya Zanzibar.

“Namwomba Mwenyezi Mungu awajalie subira, faraja na uvumilivu familia, ndugu, jamaa na wote no walioguswa na msiba huu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” amesema Dk. Mwinyi na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi.

Kwa upande wake, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanasiasa huyo, akimtaja kuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar na Tanzania.

Dk. Samia amesema kifo hicho ni pengo kwa familia na Taifa kwa ujumla, kutokana na mchango wa Mama Fatma katika vipindi mbalimbali vya historia ya Zanzibar, ikiwemo harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema Mama Fatma atakumbukwa na kuenziwa kwa mchango wake katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wa Taifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii

“Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, familia ya Hayati Sheikh Karume, ndugu, jamaa, marafiki, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote,” amesema Dk. Samia.

Aidha Dk. Samia amewaombea wafiwa na wote walioguswa na msiba huo Mwenyezi Mungu awajalie subira, faraja na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.