Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

WILAYA ya Rufiji imebainika kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko kwa kiwango cha asilimia 75, huku Mkoa wa Pwani ukikadiria zaidi ya Sh bilioni 32.6 zitahitajika kwa ajili ya maandalizi na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba mwaka huu hadi Januari 2027.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema kati ya fedha hizo, takribani Sh bilioni 17 zinahitajika kwa ajili ya Wilaya ya Rufiji, ambayo imekuwa ikikumbwa na mafuriko kutokana na historia na jiografia yake, ikiwemo athari zilizojitokeza katika msimu wa mvua wa mwaka 2023/2024.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa maendeleo, wakiwemo wawekezaji na viongozi mbalimbali mkoani Pwani, Nyongo amesema pamoja na Rufiji, maeneo mengine ni Bagamoyo, Kibiti na Kisiwa cha Mafia.

“Rufiji lipo kwenye hatari kubwa ya uhatarishi, mkoa una mahitaji ya zaidi ya Sh bilioni 32.6 kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo ikitokea, kati ya fedha hizo Sh bilioni 17 zinaelekezwa wilayani Rufiji dhidi ya athari zitakazojitokeza na kwa ajili ya tahadhari,” alibainisha Nyongo.

Kutokana na hali hiyo, Nyongo amewaagiza wakuu wa wilaya kufanya maandalizi ya mapema na tathmini za mara kwa mara katika maeneo yao ili kubaini maeneo yenye uhatarishi na kuchukua hatua kabla ya mvua hizo kuanza.

Aidha, amewataka wakuu hao kuratibu na kupokea vifaa pamoja na bidhaa mbalimbali kutoka kwa wadau, wakiwemo wawekezaji, ambao wameonyesha utayari wa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na maafa endapo yatatokea.

Amefafanua wadau hao wameonyesha utayari wa kuchangia vifaa vya uokoaji, magodoro, vyakula, vinywaji na mahema, huku akizitaka halmashauri zote kujiandaa pia kwa bajeti za dharura.

Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Romwald Mwendi, ameeleza maeneo 14 ya barabara kuu yametambuliwa na tayari yamegawanywa katika zoni nne kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji na hatua za kukabiliana na athari za mvua.

Mwendi amesema maeneo hayo yanahusisha Mkuranga, Vigwaza, Makofia na Msata, ambapo maandalizi yamefanyika kwa kuweka vifaa ikiwemo makaravati yenye urefu wa mita 500 na vikapu 300, vyenye thamani ya takribani Sh bilioni 12.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, amesema wilaya hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye historia ya kukumbwa na mafuriko, hasa katika msimu wa mvua wa mwaka 2023/2024.

Komba amesema kutokana na tahadhari iliyotolewa kuhusu mvua za El Niño, wataalamu wameandaa mpango kazi unaohusisha hatua za kuzuia athari, maandalizi na uhamasishaji wa wananchi.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kufanya siku saba za usafi wa kina kwa kushirikiana na wadau na wananchi, kufanya ukaguzi wa maeneo yenye uhatarishi pamoja na kuandaa mkutano maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari za kuchukua.

Amebainisha kuwa maeneo yaliyokwishaonekana kuwa katika uhatarishi zaidi ni pamoja na Muhoro, Umwe, Shela, Ikwiriri na Chumbi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, amesema kwa kuwa Mafia ni kisiwa, kata zote za wilaya hiyo zipo katika uhatarishi, hivyo wameendelea kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Mstaafu Joseph Kolombo, amesema wilaya hiyo imebaini maeneo hatarishi nane, yenye jumla ya kaya 5,489 na shule 12, katika kata sita zilizopo Delta ambazo zina historia ya kukumbwa na mafuriko.