Na Jackline Minja, WMJJWMM Mbeya

Zaidi ya Mama Lishe 400 wanatarajiwa kunufaika na Programu ya Mwanamke Shujaa jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, kukuza biashara na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza katika hafla ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kupitia programu hiyo iliyofanyika jijini Mbeya Septemba 21, 2026 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema programu hiyo ni mfano wa namna ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii unavyoweza kuleta matokeo katika maisha ya wananchi. 

Mhe. Mahundi amesema wanawake 160 wenye biashara watapatiwa vitendea kazi pamoja na mafunzo, huku wafanyabiashara 27 wenye mahitaji Maalum watanufaika na mpango huo.

“Ninawasihi sana wanawake wote mtakaopokea vitendea kazi hivi mhakikishe vinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa yaani kuboresha biashara, kuongeza tija, kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zenu Msiviangalie vifaa hivi kama msaada wa siku moja. Vione kama mtaji wa safari mpya ya biashara zenu.” amesema Naibu Waziri Mahundi.

Aidha Mhe. Mahundi amesema huu ni mwanzo mzuri wa jitihada kubwa za Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha biashara za wanawake, hususan Mama Lishe ambao wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

“Tunapozungumzia makundi maalum, tunajumuisha, Mama Lishe, wasusi, waendesha bodaboda na makundi mengine katika shughuli za kiuchumi, Hivyo tunapowapatia vifaa hivi, msisahau kuongeza mitaji na kutumia fursa zilizopo, ikiwemo fursa za mikopo, ili muweze kuendeleza na kukuza biashara zenu na tutahakikisha wanawake hamtoachwa nyuma katika fursa mbalimbali.” amesema Naibu Waziri Mahundi

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, amewapongeza kampuni ya Coca-Cola pamoja na kampuni ya Oryx Gas kwa kuwezesha wanawake kupitia Programu ya Mwanamke Shujaa, akieleza kuwa mpango huo umewaletea furaha wanawake walionufaika kwa kuwawezesha wanawake hao kutumia nishati safi ikiwa ni sehemu muhimu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutunza mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya , Mkuu wa Viwanda na Uwezeshaji Mkoa wa Mbeya, Festo Nasho, amesema 

kupitia ushirikiano wa kampuni ya Coca-Cola Kwanza na kampuni ya Oryx Gas imejenga na kuimarisha eneo maalum la chakula kwa Mama Lishe katika Soko la Mwanjelwa akiwasihi wanawake wanufaika kutumia fursa hiyo kwa uaminifu, kuendeleza biashara zao na kuweka akiba.