Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuna umuhimu wa kuwahamasisha vijana kujifunza zaidi kuhusu astronomia, sayansi ya anga na teknolojia, ili kuwajengea maarifa na uwezo wa kutumia fursa zinazojitokeza katika sekta hizo kwa maendeleo ya Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 21 Septemba 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Zanzibar Astronomy Space Society (ZASS), taasisi inayojihusisha na astronomia na sayansi ya anga Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amesema elimu ya astronomia, sayansi na teknolojia ina nafasi muhimu katika kuwaandaa vijana kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na kuwajengea uwezo wa kutumia maarifa hayo katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Mwinyi amesema ni muhimu kuongeza uelewa wa vijana na jamii kuhusu masuala ya anga kwa kuwapa fursa ya kujifunza, kufanya tafiti, kushiriki katika shughuli za uchunguzi wa anga na kujenga uzoefu katika matumizi ya teknolojia za kisasa.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za elimu na wadau wa sayansi na teknolojia unaweza kusaidia kuongeza hamasa miongoni mwa vijana na kufungua fursa zaidi katika utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia zinazohusiana na anga.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza ZASS kwa juhudi zake za kuhamasisha astronomia na sayansi ya anga, hususan kwa vijana, na kueleza umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano utakaosaidia kuongeza uelewa na maarifa katika fani hizo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhiwa picha mbalimbali za astronomia zilizopigwa kutoka Zanzibar na Chama hicho, zinazoonesha baadhi ya maumbo na mandhari ya anga za mbali, ikiwa ni sehemu ya shughuli za taasisi hiyo katika uchunguzi na upigaji picha za anga.

Naye Abuubakar Harith Msemaji wa ZASS amesema matumizi ya satelaiti yanaweza kutoa mchango mkubwa katika tafiti na upatikanaji wa taarifa zinazoweza kusaidia mipango ya maendeleo ya Zanzibar.
Amesema teknolojia hizo zinaweza kutumika katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa zinazohusu bahari, mazingira na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani.