Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 21, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Shirika hilo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 Shirika hilo limepata faida ya takriban shilingi bilioni 73 na kulipa kodi zote zenye thamani ya shilingi bilioni 50.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Septemba 21, 2026, kuhusu utekelezaji wa TPDC katika mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27, amesema kutokana na mapato ya gesi asilia, Shirika limepeleka serikalini shilingi bilioni 142 ikiwa ni mgao wa faida ya gesi pamoja na mrahaba.
Aidha, amesema TPDC imelipa gawio la shilingi bilioni 15, hivyo kwa ujumla kiasi ambacho Shirika hilo limepeleka au kulipa serikalini katika mwaka huo wa fedha kinafikia shilingi bilioni 207.
Amesema mafanikio hayo ni miongoni mwa viashiria vinavyoonyesha kuwa TPDC inaendelea vizuri katika operesheni zake, kutekeleza majukumu yake na kuendelea kujipanga kuongeza zaidi mafanikio yaliyofikiwa katika mwaka huo.
Kwa upande wa uzalishaji wa gesi asilia, amesema kwa sasa shughuli hizo nchini zinafanyika katika vitalu viwili ambavyo ni Songosongo kinachoendeshwa na Pan African Energy Tanzania (PAET) na Mnazi Bay kinachoendeshwa na Maurel & Prom (M&P).
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, uzalishaji umeendelea kwa wastani wa futi za ujazo milioni 170 kwa siku, huku takriban asilimia 85 ya gesi hiyo ikitumika kuzalisha umeme unaouzwa kwa TANESCO.
Pia ameongeza kuwa kiasi kingine cha gesi kinatumika viwandani, majumbani, kwenye taasisi na katika vyombo vya moto hususan magari na bajaji kupitia mfumo wa CNG.
Akizungumzia miradi mikuu iliyotekelezwa, amesema utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga, umefikia asilimia 92.7.
Amesema kwa sasa wanatarajia kuanza kuingiza mafuta kwenye bomba hilo mwezi Desemba mwaka huu, baada ya ratiba kusogezwa kutokana na changamoto kadhaa, hususan kuchelewa kwa baadhi ya vifaa na vipuri kutoka maeneo ya Mashariki ya Kati kutokana na vita.
Aidha, amesema TPDC imetekeleza uchorongaji wa visima vitatu vipya katika kitalu cha Mnazi Bay, ambapo visima viwili vimekamilika kwa mafanikio na kuongeza uwezo wa uzalishaji kwa futi za ujazo milioni 65 kwa siku, kutoka takriban milioni 110 zilizokuwa zikizalishwa awali.
Ameongeza kuwa kisima cha tatu kimekamilisha sehemu ya uchorongaji na matokeo yake bado yanakusanywa na kutafsiriwa, hivyo TPDC itatangaza matokeo rasmi baada ya kupata taarifa kamili, huku visima hivyo vitatu vikitarajiwa kuongeza uzalishaji wa Mnazi Bay hadi angalau futi za ujazo milioni 150 kwa siku.
