Askofu mkuu mwangalizi wa makanisa ya Wabatisti Tanzania,Askofu Anold Manase wakati akizungumza katika mahafali hayo

Na Happy Lazaro, Arusha
Wazazi pamoja na walezi wametakiwa kuendelea kuwafuatilia watoto wao kwani kuhitimu darasa la saba sio kuhitimu maisha wala malezi kwani bado wana nafasi kubwa ya kuwafuatilia mpaka watakapofikia hatua ya wao kujitegemea.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Askofu mkuu mwangalizi wa makanisa ya Wabatisti Tanzania,Askofu Anold Manase wakati akizungumza katika mahafali ya ya darasa la saba katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya Maromboso Baptist iliyopo kata ya Ngarenaro jijini Arusha .
Askofu Manase amesema kuwa,wazazi na walezi bado wana nguvu ya kuwekeza kwa watoto wao kwa kupewa malezi ya kijimudu wenyewe ili waweze kujitegemea kwa maisha yao ya baadaye.
“Nawaombeni sana wazazi na walezi muendelee kuwafuatilia watoto wenu kwa karibu kwani wanahitaji uangalizi mkubwa ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kujiepusha na makundi yasiyofaa ambayo mwisho wa siku yanawaharibia maisha yao .”amesema Askofu Manase.
“Kuwekeza kwa mtoto ni.kuwekeza katika maisha yake ya leo na ya baadaye na ni lazima watoto wafundishwe kazi za mikono ambazo zitawafanya wajue pia uhalisia wa maisha .”amesema Askofu Manase.
Aidha Askofu Manase amewapongeza wazazi kwa kuwekeza katika elimu kwani huo ni urithi ambao watakuwa nao na elimu iliyowekwa ndani yake hawawezi kuitupa kwani urithi wa kwanza wa kuwapa watoto ni Mungu ,elimu
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa shule hiyo,Jackson Joseph amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikiwaandaa watoto kiroho na kimwili ambapo imekuwa ikitoa elimu kwa vitendo zaidi na kuwawezesha kuwa wabunifu na hata kuweza kujitegemea.
Aidha amesema kuwa,kitaaluma shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika masomo yake katika matokeo ya darasa la saba mfululizo ambapo idadi kubwa ya wanafunzi ambao wamekuwa wakihitimu shuleni hapo wamefanikiwa kuwa katika nafasi kubwa katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Janeth Shayo amewapongeza wazazi kwa kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao kwani huo ndio urithi pekee anaotakiwa kupewa mtoto kwa ajili ya maisha yake ya baadaye .
“Nawaombeni wazazi waendelee kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza shule yetu katika maeneo mbalimbali watakapokuwa ili waweze kuleta wanafunzi shuleni hapa kutokana na elimu bora ambayo imekuwa ikitolewa na walimu wazuri na waliobobea .”amesema Shayo.
