Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali na taasisi za dini zina wajibu wa kuendelea kushirikiana katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano, kukuza maadili mema na kuchangia ustawi wa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 20 Septemba 2026, katika Ibada ya kumweka Wakfu na Kumketisha Kitini Askofu wa 11 wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar, Mhashamu Askofu Lameck Paul Ndomba, hafla iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini una nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye maelewano na mshikamano, huku taasisi hizo zikiwa na mchango mkubwa katika elimu, afya, malezi, ujenzi wa maadili na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kusikiliza na kushirikiana na viongozi wa dini katika masuala yenye maslahi kwa wananchi, akieleza kuwa mchango wa taasisi za dini hauishii katika huduma za kiroho pekee, bali unagusa pia maisha na maendeleo ya jamii.
Amesema tofauti za kiimani hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko, bali ziwe msingi wa kuheshimiana, kuvumiliana na kushirikiana katika kudumisha amani na kuendeleza maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumzia matumizi ya lugha ya Kiswahili, Rais Dkt. Mwinyi amelipongeza Kanisa la Anglikana kwa kuendelea kutumia na kukiendeleza Kiswahili katika mikutano na shughuli zake, akieleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za kukuza matumizi ya lugha hiyo ndani na nje ya nchi.
Amesema hadhi ya Kiswahili imeendelea kuimarika katika ngazi za kikanda na kimataifa, ambapo ni miongoni mwa lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, pamoja na kuwa lugha rasmi ya kazi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akimpongeza Mhashamu Askofu Lameck Paul Ndomba, Rais Dkt. Mwinyi amesema uteuzi wake ni dhamana kubwa ya kuiongoza Dayosisi ya Zanzibar, na amemtakia hekima, busara na nguvu katika kutekeleza majukumu yake ya kiuchungaji na kulitumikia Kanisa kwa uadilifu.
Rais Dkt. Mwinyi pia amempongeza Mhashamu Askofu Mkuu kwa juhudi za kuimarisha maelewano na kurejesha utulivu ndani ya Kanisa, akieleza kuwa kusameheana, kuvumiliana, kupendana na kujenga umoja ni miongoni mwa misingi muhimu ya mafundisho ya Kikristo.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa la Anglikana katika kuhifadhi, kutunza na kuendeleza maeneo ya kihistoria, kutokana na umuhimu wake katika kuhifadhi historia ya Zanzibar, kutoa elimu kwa wananchi na wageni pamoja na kukuza utalii wa kihistoria na kiutamaduni.
Akizungumzia hali ya hewa, Rais Dkt. Mwinyi amehimiza wananchi kuchukua tahadhari na kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu mvua za Vuli zinazotarajiwa kuathiriwa na hali ya El NiƱo.
Amehimiza pia viongozi wa dini kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa, sambamba na kumuomba Mwenyezi Mungu mvua hizo ziwe za heri na baraka na kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amemkaribisha Mhashamu Askofu Lameck Paul Ndomba Zanzibar na kumtakia hekima, afya, nguvu na neema ya Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza Dayosisi ya Zanzibar.
Naye, Mhashamu Askofu Lameck Paul Ndomba, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa ushirikiano anaouonesha kwa taasisi za dini, pamoja na juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

