Zanzibar, Septemba 18, 2026 – Kampeni ya Tumaini ya Yas Tanzania imefika Zanzibar, ambapo kampuni hiyo imekabidhi vifaa vya uzazi katika Hospitali ya Wilaya ya Mwera Pongwe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda vya uchunguzi kwa wajawazito, viti mwendo, mashuka, vifaa vya kujifungulia (delivery trays) pamoja na khanga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Mhe. Rajab Ally Rajab, aliipongeza Yas kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya, hususan huduma za mama na mtoto.
“Tunathamini ushirikiano huu kwa sababu vifaa hivi vinakwenda moja kwa moja kusaidia huduma zinazotolewa kwa akina mama katika hospitali yetu. Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya, na tunapopata wadau wanaokuja kuunga mkono juhudi hizi, inatupa fursa ya kuboresha huduma kwa wananchi wetu,” alisema Mhe. Rajab.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hospitali hiyo, Dkt. Pathan Mohamed Pathan, amesema upungufu wa vifaa tiba ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili hospitali hiyo, huku takribani kina mama wajawazito 300 wakipatiwa huduma za kujifungua hospitalini hapo kila mwezi.
“Kwa mwezi tunahudumia takribani kina mama wajawazito 300 wanaokuja kujifungua hapa hospitalini. Idadi hii ni kubwa na inahitaji kuwa na vifaa vya kutosha ili tuweze kutoa huduma bora na salama kwa mama na mtoto. Msaada huu umekuja wakati muafaka na utatusaidia sana katika kuboresha huduma zetu,” amesema Dkt. Pathan.
Kwa upande wake, Mkuu wa Yas Zanzibar, Mohamed Waqid, alisema msaada huo ni sehemu ya Kampeni ya Tumaini inayolenga kuboresha mazingira ya huduma kwa akina mama wajawazito na kuwawezesha watoa huduma za afya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Safari ya mama mjamzito hadi kujifungua inahitaji uangalizi, huduma nzuri na mazingira salama. Tunataka vifaa hivi viwasaidie madaktari na wauguzi kufanya kazi zao vizuri zaidi, na kumsaidia mama anayefika hapa akiwa na matumaini ya kujifungua salama na kurudi nyumbani pamoja na mtoto wake,” alisema Waqid.
Aliongeza kuwa Kampeni ya Tumaini ni sehemu ya dhamira ya Yas kugusa maisha ya jamii inayoihudumia na kwamba kwa Zanzibar, Yas imeendelea kuwekeza katika huduma za mawasiliano, huku mtandao wake ukiwafikia takribani asilimia 99 ya wakazi, sambamba na kuwekeza katika programu za kijamii.
“Tunaposema Yas ni Mtandao wa Viwango, hatuzungumzii ubora wa mawasiliano pekee, bali pia namna tunavyoshirikiana na jamii na kuchangia maendeleo yake,” alisema.
Waqid alisema Kampeni ya Tumaini itaendelea kufika maeneo mengine ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya jitihada za kampuni kusaidia kuboresha huduma za mama na mtoto.
