Wathamini wamemuaga kwa heshima Mthamini Mkuu Bi. Eveline Mugasha kwa mbio maalumu (jogging) ya kilomita tano, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi na kumpongeza baada ya kustaafu utumishi wa Umma.
Jogging hiyo imefanyika leo, Jumamosi, Septemba 19, 2026, ikiwa ni ishara ya heshima, mshikamano na kuthamini mchango wa Bi. Mugasha katika utumishi wa umma na taaluma ya uthamini.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Mugasha amewashukuru Wathamini wenzake kwa kumuaga kwa namna ya kipekee, akieleza kuwa jogging hiyo imekuwa kumbukumbu muhimu kwake katika hatua ya kustaafu utumishi wa umma.
Akiwa miongoni mwa washiriki wa jogging hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Eleuteri Mangi, amempongeza Bi. Mugasha kwa utumishi wake, akieleza kuwa bado wanatarajia kuendelea kupata ushirikiano na uzoefu wake katika masuala mbalimbali kwenye Sekta ya Ardhi.
Bw. Mangi amewapongeza Wathamini kwa kuendelea kushirikiana katika kufanya mazoezi ya pamoja, akisisitiza umuhimu wa watumishi kuendelea kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi kwa ajili ya afya na ustawi wao.
Kwa upande wake, Gerson Marisa kutoka Kampuni ya Uthamini ya TKA Company Limited, amesema Bi. Mugasha amekuwa na historia nzuri ya kuwaunganisha Wathamini kutoka kampuni binafsi na Serikali, pamoja na kujenga mshikamano na kufanya kazi kama timu.
Naye Sharifa Issa kutoka Kitengo cha Ardhi, amesema watumishi wataendelea kutumia na kuenzi mambo mema waliyojifunza kutoka kwa Bi. Mugasha, ikiwa ni moja ya njia za kuhifadhi na kuendeleza urithi wake wa kitaaluma.
Jogging hiyo imewakutanisha Wathamini kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wathamini kutoka kampuni binafsi za uthamini, katika kumuaga na kumpongeza Bi. Mugasha kwa hatua yake ya kustaafu utumishi wa umma.

