Mwamvua Mwinyi, Pwani

Septemba 18, 2026

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo (Mb), amewaagiza Makamishna wa Ardhi wa mikoa nchini kufanya ukaguzi wa maeneo ya ardhi yaliyotolewa kwa ajili ya uwekezaji, ili kubaini wawekezaji waliohodhi ardhi pasipo kuziendeleza.

Ameeleza taarifa ya idadi ya wawekezaji watakaobainika kumiliki pasipo kuyaendeleza kinyume na masharti ya umiliki wa ardhi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa Serikali haitaki ardhi iliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji kubaki bila muendelezo.

Akwilapo ametoa maagizo hayo Septemba 18, 2026, wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, akikagua maeneo yaliyotolewa kwa ajili ya uwekezaji katika Kongani ya Viwanda ya Modern Industrial Park-KAMAKA na Kongani ya Gaini.

Aidha, amewataka wamiliki wa ardhi kuyaendeleza maeneo yao badala ya kuyaacha bila matumizi na hatimaye kusababisha migogoro ya ardhi, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Kadhalika ameeleza hadi sasa Serikali imeshatoa hati miliki na hati za kimila 600, hatua inayolenga kuwawezesha wawekezaji kutumia ardhi kwa uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Akwilapo amesema atasimamia changamoto ya baadhi ya wawekezaji kutoka nje kununua viwanja moja kwa moja kutoka kwa wananchi wanaouza ardhi kiholela, akisema hali hiyo inaweza kusababisha kuchanganyika kwa maeneo ya uwekezaji na makazi kinyume na taratibu.

“Tunaagiza kutengwa kwa maeneo ya uwekezaji ili kurahisisha utoaji huduma wezeshi kwa wawekezaji wa viwanda,Tunataka kuona mambo haya yanakuwa sawa na wawekezaji wafuate taratibu na sheria zilizopo,” anasema. 

Mkurugenzi KAMAKA, Yusuph Manzi, ameeleza kuvutia wawekezaji kunakabiliwa na changamoto kutokana na baadhi ya wawekezaji kununua maeneo ya wananchi yanayouzwa kwa gharama nafuu badala ya kuwekeza katika maeneo yaliyotengwa rasmi.

Meneja wa KAMAKA, Sadock Nshekanabo, amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh trilioni 3.5 na una jumla ya viwanja 202, viwanja saba tayari viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Amefafanua miongoni mwa changamoto zinazokabili kongani hiyo ni upatikanaji wa maji na ubovu wa barabara ya kilomita 23 inayoelekea eneo hilo, hali inayosababisha kero katika usafirishaji wa bidhaa na malighafi.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Samwel Mwambungu, amesema tayari mkandarasi amepatikana kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, huku hatua za muda mfupi zikichukuliwa kwa kuweka mawe katika maeneo korofi ili yaweze kupitika wakati wa mvua.

Nae Barnabas Taligunga kutoka DAWASA Kibaha ameelezea changamoto ya maji inafanyiwa kazi, huku akieleza kuwa Sh milioni 934 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji utakaodumu kwa miezi sita na kukamilika Machi 2027.