Na Mwandishi wetu, Nzega
MWENGE wa uhuru unatarajiwa kuzindua, kukagua, kutembelea na kuweka jiwe la msingi, kwenye miradi ya thamani ya shilingi bilioni 4.1 Wilayani Nzega Mkoani Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega Naitapwaki Tukai ameeleza hayo wakati akikabidhiwa mwenge wa uhuru na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui Pendo Wella ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora.
DC Tukai amesema ukiwa Wilayani Nzega, mwenge wa uhuru utakimbizwa umbali wa kilometa 223 na kupitia miradi ya thamani ya shilingi bilioni 4.1 ambapo Nzega DC thamani yake ni shilingi bilioni 1.2 na Nzega mji shilingi bilioni 2.9.
Amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa maeneo ambayo yamepitiwa na mwenge kwani wamekuwa na hamasa kubwa na mwamko pindi ukipita na kujitokeza kwa wingi kwenye mkesha kata ya Nata.
“Tangu niteuliwe na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa DC Nzega miaka minne iliyopita sijawahi kuwaona pamoja wabunge wa majimbo ya Nzega vijijini na Bukene wakiwa pamoja ila leo nimewaona na nimefurahi mno,” amesema DC Tukai.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Michael amempongeza DC wa Nzega Naitapwaki Tukai kwa namna alivyosimamia maendeleo ya eneo hilo.
“Leo tumeingia Nzega DC kutoka Uyui na tangu tulivyoanza mradi wa kwanza hadi wa mwisho yote ni mizuri na kesho Nzega mji nasikia mambo ni mazuri huko hongera sana Mkuu wetu wa Wilaya,” amesema.
Amewaasa wana Nzega waendelee kumpa ushirikiano wa kutosha mkuu wao wa Wilaya ambaye anamwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye eneo hilo.
Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 kutoka mkoa wa Manyara, Inyasi Amsi amempongeza DC Naitapwaki Tukai kwa namna anavyosimamia maendeleo na ushirikiano kwa wana Nzega.
“Hakika Mheshimiwa DC unatuheshimisha wana Manyara kwani watu wa hapa Nzega wanakupenda kutokana na namna unavyowaongoza na kuwasimamia,” amesema Inyasi.
