Na. Meleka Kulwa-FullshangweBlog, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, amemtaka mkandarasi wa mradi wa Soko la Majengo kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, huku akibainisha Kuwa muda wa nyongeza aliopewa hautaongezwa tena, aidha amemtaka mkandarasi wa Stendi ya Kizota kuongeza kasi ya kazi ili mradi ukamilike ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba 2026.
Ametoa maelekezo hayo Septemba 16, 2026, Jijini Dodoma, wakati akiongoza Kamati Tendaji ya Mkoa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Jiji la Dodoma, ikiwemo ujenzi wa Stendi mpya ya Mnada mpya kata ya Kizota, Soko la Majengo na Makao Makuu ya TBC eneo la Vikonje.
Amebainisha kuwa kazi iliyokuwa kwenye mpango wa awali inapaswa kukamilishwa kwa uhalali wake, huku kazi za nyongeza zikitenganishwa na kutekelezwa kulingana na muda uliotolewa.
Aidha, amesema kasi ya utekelezaji inapaswa kuongezwa kwa kutumia muda wa mchana na usiku, akibainisha kuwa Serikali haijapata malalamiko kuhusu upatikanaji wa fedha za mradi huo.
Ameongeza kuwa kutokana na matarajio ya mvua nyingi zinazohusishwa na El Niño, ni muhimu kazi hizo kuharakishwa ili majengo yakamilike kabla ya mvua kuanza.
Pia amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kusafisha Mto Pombe, akibainisha kuwa hatua ya kusafishwa kwa sehemu ya korongo hilo ni muhimu katika maandalizi ya kukabiliana na mvua zinazotarajiwa.
Kwa upande wa mradi wa Makao Makuu ya TBC, Senyamule amesema ni miongoni mwa miradi ya kimkakati katika Mkoa wa Dodoma, huku akibainisha kuwa ujenzi wa jengo hilo unavutia na kasi yake inaridhisha.
Ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi zinazotekeleza miradi hiyo ili kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, mkandarasi wa mradi wa Soko la Majengo amebainisha kuwa mpango wao ni kukamilisha kazi zote ambazo bado hazijakamilika ndani ya siku 60.
Huku Mhandisi na maratibu wa Miradi ya TACTIC Nicodemus Kileo, amesema mradi wa stendi ya mnada mpya umefikia asilimia 38 ya utekelezaji.
Naye Mwenyekiti wa Soko Kuu la Majengo, Godson Lugazama, ameishukuru Serikali kwa kuruhusu mradi wa ukarabati kufanyika katika soko hilo.
Pia, amebainisha kuwa ushirikishwaji wa wafanyabiashara katika utekelezaji wa mradi huo umeleta tija, akiongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mkoa, Wilaya, Halmashauri ya Jiji na wafanyabiashara umewezesha kufikia hatua iliyopo sasa.

