Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk. Jim Yonazi, amesema uratibu wa kisera na utekelezaji wa mipango kwa pamoja ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dk. Yonazi ameyasema hayo Septemba 16, 2026, Jijini Arusha wakati akizungumza katika Kongamano la WanaMipango 2026, ambapo ameeleza kuwa Tanzania ina jumla ya sera 64, kati ya hizo sera 12 zikiwa katika mchakato wa mapitio na sera nyingine sita zikiwa zimeandaliwa kwa ajili ya matumizi nchini.
Amesema sera hizo zinapaswa kuanishwa na kuonesha matamko ya Serikali katika sekta mbalimbali ili taasisi zitekeleze majukumu kwa pamoja na kuweka mkono malengo ya Taifa, ikiwemo kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Kwa mujibu wa Dk. Yonazi, Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu na kuoanisha sera pamoja na kuifuatilia Serikali kupitia taarifa za utekelezaji zinazotolewa na taasisi mbalimbali.
Amesema uratibu huo unasaidia kupima hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mipango kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka mifumo madhubuti ya utekelezaji na ufuatiliaji.
Aidha, Dk. Yonazi amesema Miongozo ya Utekelezaji wa Dira ya 2050 inawawezesha wanamipango kuoanisha mipango ya miaka mitano, ilani za vyama na mipango mikubwa ya Taifa, na hivyo kusaidia kuimarisha ushirikiano na uratibu miongoni mwa taasisi za Serikali na sekta binafsi katika kufikia malengo ya Taifa.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali pamoja na uratibu madhubuti ili kuhakikisha mipango na sera za Taifa zinakwenda sambamba na malengo ya maendeleo ya Tanzania.


