Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx Tanzania, Angelica Pesha (wa pili kulia), na Mratibu wa Jukwaa la Asasi za Kiraia Zanzibar (ZANGOF), Dkt. Mahfoudh Hassan Haji (katikati), wakionesha hati za makubaliano ya ushirikiano ambayo yatapanua upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kwa asasi za kiraia katika tukio lililofanyika leo visiwani humo. Wanaoshuhudia ni Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Khalid Abdalla (wa pili kushoto), Mkuu wa Yas – Zanzibar, Mohamed Waqid (kulia) na Mwenyekiti wa ZANGOF Ndugu Hassan Hamis Juma (kushoto). Kupitia ushirikiano huo, wanachama wa ZANGOF wataweza kutumia Mixx Business Suite kufanya malipo na miamala mingine ya kifedha kidijitali.

…………

Zanzibar, Septemba 16, 2026 – Asasi za kiraia Zanzibar zitapata fursa ya kutumia huduma za kifedha za kidijitali kusimamia malipo, mishahara na fedha za taasisi kwa urahisi na uwazi zaidi, kufuatia makubaliano ya ushirikiano kati ya Mixx na Jukwaa la Asasi za Kiraia Zanzibar (ZANGOF). 

Makubaliano hayo yatawezesha asasi zilizo chini ya ZANGOF kutumia huduma ya Mixx Business Suite kufanya malipo ya mishahara na wanufaika, pamoja na kusimamia miamala mingine ya taasisi kwa njia ya kidijitali. Asasi hizo pia zitaweza kupata huduma za mawasiliano na intaneti za Yas. 

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo Zanzibar, Mrajisi Mkuu wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Khalid Abdalla, alisema matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia asasi kuboresha usimamizi wa fedha na utoaji wa huduma kwa wananchi. 

“Asasi za kiraia zinafanya kazi moja kwa moja na wananchi katika maeneo mbalimbali. Tunataka kuona teknolojia ikitumika kurahisisha kazi zao, kuongeza uwazi katika usimamizi wa fedha na hatimaye kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi,” alisema Abdalla. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema ushirikiano huo utasaidia kupeleka huduma za kifedha za kidijitali karibu zaidi na asasi pamoja na jamii wanazozihudumia. 

“Asasi hizi zinafanya kazi na wanawake, vijana, wajasiriamali na makundi mbalimbali katika jamii. Kupitia huduma zetu, tunataka kuwapa njia rahisi na salama zaidi za kusimamia fedha, kufanya malipo na kuweka akiba. Kwetu, ujumuishaji wa kifedha ni kuona huduma hizi zikimsaidia mwananchi kuboresha shughuli na maisha yake,” alisema Pesha. 

Makubaliano hayo pia yanatoa fursa kwa vikundi vinavyofanya kazi na asasi za kiraia kutumia Kikoba cha Mixx, kinachowawezesha wanachama kuweka akiba, kuchangia, kununua na kuuza hisa pamoja na kukopeshana kwa njia ya kidijitali. 

Mixx tayari inashirikiana na taasisi mbalimbali Zanzibar katika matumizi ya huduma za kidijitali, zikiwemo Idara ya Maendeleo ya Ushirika, ZARTSA, ZanBus na ZSTC, katika maeneo kama malipo ya wakulima, usafiri wa umma na huduma nyingine. 

Makubaliano na ZANGOF yanatarajiwa kupanua matumizi ya huduma hizo kwa asasi za kiraia na vikundi vya kijamii Zanzibar.