WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ndani ya wiki moja, Serikali itachukua hatua ya kuhakikisha bei ya saruji inakuwa himilivu kwa wananchi, baada ya kubaini malalamiko ya kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Simiyu.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Septemba 15, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Bariadi Mjini, mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Saba Saba.
“Serikali tumeliona hilo. Serikali sikivu tumesikia hilo. Nimewatuma wataalamu ndani ya wiki moja wawe wameshapata ufumbuzi. Tutatoa tamko la njia ya kushusha bei ya saruji ili kila Mtanzania aweze kumudu. Katika baadhi ya maeneo bei ya saruji imefikia zaidi ya sh. 26,000 na katika baadhi ya mikoa ya mipakani imefikia sh. 32,000,” amesema na kusisitiza kuwa Serikali inataka wananchi waweze kumudu gharama za ujenzi wa nyumba na miradi mingine ya maendeleo.
Kuhusu zao la pamba, Waziri Mkuu amesema ameielekeza Wizara ya Kilimo ikutane na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja na ifikapo Oktoba 15, 2026 apelekewe mapendekezo rasmi kuhusu bei na mfumo bora wa ununuzi wa zao hilo ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi.
“Nimeipokea hoja hii. Nimeelekeza Wizara ya Kilimo ikae na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja. Ifikapo tarehe 15 mwezi wa 10, niwe nimeshapata mapendekezo rasmi yaliyorejea mifumo ambayo tumeshaitumia na kubaini upi ni mfumo bora ili tuweze kuhakikisha kwamba wakulima wananufaika,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema pia Serikali imebadilisha utaratibu wa kodi kwa wenye biashara mpya, ambapo mfanyabiashara anayeanzisha biashara atapewa muda wa kuimarisha biashara yake kabla ya kuanza kubeba mzigo wa kodi. “Zamani ilikuwa mtu akianzisha tu biashara, siku hiyo hiyo anaanza kudaiwa kodi. Sasa tumefuta, atasubiriwa mwaka mzima ili biashara yake iimarike,” amesema.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga uchumi shirikishi, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kutekeleza sehemu kubwa ya shughuli za maendeleo.
Mapema, akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, amemshukuru Waziri Mkuu kwa ziara hiyo na kueleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo inayogusa sekta za maji, elimu, afya na barabara.
Mhandisi Kundo amesema mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya sh. bilioni 440 unaendelea kutekelezwa mkoani humo, huku Serikali ikiwa imetoa sh. milioni 460 kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Majaida–Munambala katika Mto Ndoba.
Kuhusu ujenzi wa soko la kisasa la Bariadi mjini, Mhandisi Kumndo amesema ujenzi wake unaendelea, huku akiomba kasi ya mkandarasi iongezwe ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Akigusia barabara za Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo amesema Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha kilomita zote 8.6 zilizotengewa ujenzi zinajengwa kwa awamu mbili, ambapo kilomita tano zitajengwa katika awamu ya kwanza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amesema Serikali ya Mkoa itasimamia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu wakati wa ziara hiyo na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Maagizo na maelekezo yako uliyoyatoa katika ziara yako hii tunayasimamia, tuyatekeleze, na kuleta ripoti ya utekelezaji katika ofisi yako ya Waziri Mkuu,” amesema.

