Dodoma, Septemba 15, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amepokea vifaa vya uchunguzi wa wanawake wajawazito kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika vituo vya afya ngazi ya msingi mkoani Dodoma.

Teknolojia hiyo inatarajiwa kusaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa ‘ultrasound’ kwa kuwawezesha watoa huduma za afya waliopata mafunzo, ambao si wataalamu wa ‘ultrasound’, kufanya uchunguzi wa awali kwa usahihi na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.Mhe. Senyamule amesema hayo leo, Septemba 15, 2026, wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika katika Kituo cha Afya Mkonze, jijini Dodoma. Vifaa hivyo vitatumika katika vituo 32 vya afya ngazi ya msingi vinavyoshiriki katika Mradi wa Utafiti wa Uwezekano wa Matumizi ya ‘Ultrasound’ Inayosaidiwa na Akili Unde na Tathmini ya Rasilimali na Ujumuishaji (SAFARI) unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema mradi huo unalenga kutathmini namna teknolojia ya Akili Unde inavyoweza kuunganishwa kikamilifu katika utoaji wa huduma za kawaida za afya ya mama na mtoto katika ngazi ya msingi.

“Teknolojia hii ina uwezo wa kusaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa ‘ultrasound’ kwa kuwawezesha watoa huduma ambao si wataalamu wa ‘ultrasound’ kufanya uchunguzi wa awali kwa usahihi wa hali ya juu,” amesema Mhe. Senyamule.

Aidha, amesema upungufu wa wataalamu wa ‘ultrasound’ ni changamoto ya kitaifa na kimataifa, hususan katika nchi zinazoendelea. Ameongeza kuwa Mradi wa SAFARI hauishii katika utoaji wa vifaa pekee, bali unahusisha pia mafunzo kwa watoa huduma, uhakiki wa ubora, usimamizi na tathmini endelevu ya matumizi ya teknolojia hiyo na matokeo yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, amesema Kituo cha Afya Mkonze kimechaguliwa kuwa kituo cha mfano, akisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema katika kubaini changamoto za kiafya na kuboresha matokeo ya matibabu pamoja na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Naye mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. James Kiengia, amesema zaidi ya asilimia 83 ya Watanzania hupata huduma za afya kupitia vituo vya afya ngazi ya msingi, hivyo kuonesha umuhimu wa kimkakati wa kutekeleza Mradi wa SAFARI katika ngazi hiyo.

Mradi wa SAFARI ni wa miezi 18, unaotekelezwa kuanzia Januari 2026 hadi Juni 2027 katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Dodoma, ambao umechaguliwa kuwa eneo la majaribio (pilot area) la mradi huo.

Mradi huo unatekelezwa na UDOM kwa kushirikiana na ‘Liverpool School of Tropical Medicine’ (LSTM), kwa ufadhili wa Gates Foundation, chini ya usimamizi wa kisera wa Wizara ya Afya.

Mradi tayari umefanya tathmini ya awali katika vituo vyote 32 vinavyoshiriki pamoja na hospitali zao za rufaa, kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa vya utekelezaji.