Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi John Ulanga, amekutana na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) kutoka nchi mbalimbali wanachama wa EU katika Ofisi Ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam, kujadili maandalizi ya EU–Tanzania Investment and Business Roadshow 2026–2027.
Mazungumzo hayo yalilenga maandalizi ya mfululizo wa Roadshow utakaofanyika katika nchi za Finland, Italia na Uholanzi, kwa kushirikiana na Ubelgiji, kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 6 Oktoba 2026, ikiwa ni hatua ya awali kuelekea EU–Tanzania Investment and Business Forum itakayofanyika Dar es Salaam mapema mwaka 2027.
Mpango huu unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa kuwaleta pamoja Serikali, wawekezaji, wafanyabiashara, taasisi za fedha na sekta binafsi, kwa lengo la kutambua fursa, kujenga ubia na kuvutia uwekezaji wenye tija nchini Tanzania.
Mkutano huo pia ulisisitiza umuhimu wa maandalizi ya pamoja na uratibu wa karibu ili kuhakikisha Roadshow inakuwa jukwaa la kuunganisha fursa za Tanzania na mitaji, teknolojia, utaalamu na masoko ya Ulaya, huku ikiimarisha zaidi mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

