Zaidi ya wagonjwa 500 hutibiwa magonjwa ya saratani katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.
Hayo yamebainishwa na Dkt Tibera Rugambwa Kaimu kitengo cha saratani Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya inayohudumia mkikoa saba ya Mbeya,Iringa, Njombe,Songwe,Ruvuma,Rukwa na Katavi wakati wa kupokea msaada wa vifaa tiba na dawa kutoka kwa Jema Baruani Mkurugenzi wa Taasisi ya Jema Foundation.
Tibera amesema tatizo la saratani ni kubwa katika kanda yake na ametoa wito kwa wananchi kufika mapema hospitali ili kupata matibabu mapema.
“Naipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuanzisha kitengo cha saratani kwa miaka miaka mitano sasa ambapo wananchi sasa wanaweza kupata matibabu kwa haraka na gharama nafuu”alisema Tibera.
Akitoa msaada huo Jema Baruani Mkurugenzi wa Jema Foundation amesema amewiwa kutoa msaada huo kwa lengo la kuwatia moyo na matumaini wagonjwa wa saratani kuwa satatani inatibika na kwamba waachane na mila potofu kwenda kwa waganga wa kienyeji wakidhani wamelogwa.
Jema ambaye ni shujaa wa sarani aliyeishi na ugonjwa huo kwa miaka tisa amewaomba wadau wengine kuungana na Taasisi yake ili kuwasaidia wagonjwa wa saratani kwani gharama za vipimo na matibabu yake ni aghali sana.
Akipokea msaada huo Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt Awesu Mchepange amemshukuru Jema Baruani kwa msaada alioutoa ambapo ametoa wito kwa wananchi kufika hospitali huduma ambazo awali zilikuwa zikipatikana nje ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini hususani Ocean Road Dar es Salaam.
Amesema kwa sasa wananchi wamepunguziwa gharama kubwa ambazo walikuwa wakizitumia kwa kusafiri umbali mrefu.
Aidha amewataka wadau wengine kuungana ili kusaidia wagonjwa wa saratani kwani gharama za vipimo na dawa ni aghali sana kwa watu wengine wa kipato cha chini hawawezi kuzimudu.
Mwakilishi wa Ocean Silent Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati Gilbert Nyangwe amesema wao ni wadau wakubwa wa afya na ushirikiano walionao na Jema Foundation umewawezesha Watanzania wengi kutibiwa hususani hospitali za Serikali ambazo hutumia mfumo wake wa fedha(control number).
Amezitaka Taasisi nyingine kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jema Foundation ili kuokoa maisha ya Watanzania ambao hawawezi kugharamia matibabu ya saratani ambayo ni aghali.
Judith Mwakalinga ni shujaa wa sarani kwa niaba ya wagonjwa wa saratani ameishukuru Taasisi ya Jema Foundation kwa msaada wa dawa na vifaa tiba kwani vitaongeza ari ya utendaji kwa wafanyakazi wa Hospitali.
Awali katika ufunguzi wa hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa utawala rasilimali watu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya amesema milango ipo wazi kwa wadau kutoa misaada kusaidia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Jema Baruani amehitimisha hafla hiyo kwa kuwatembelea wagonjwa wa saratani na kuwagawia zawadi huku akiwatia moyo wagonjwa wasikate tamaa kwani saratani inatibika.

