*Ukosefu wa mawasiliano chanzo cha mgogoro wa wabia katika leseni 33
*Wachimbaji watakiwa kuweka mifumo ya wazi ya ushirikiano na mawasiliano
*Serikali yaonya leseni zisizoendelezwa kufutwa
Mwanza
Ukosefu wa Mawasiliano na taarifa sahihi miongoni mwa wamiliki wa leseni za uchimbaji madini unaweza kuchochea migogoro isiyo ya lazima na kudhoofisha shughuli za uchimbaji, hasa kwa wachimbaji wadogo.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 15, 2026 jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akiongoza kikao cha kutatua mgogoro uliowahusisha wachimbaji wadogo jijini humo.
Dkt. Kiruswa amesema mgogoro huo umetokana kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa taarifa sahihi na mawasiliano baina ya wabia wanaomiliki kwa pamoja leseni 33, ambapo upande mmoja uliamini kuwa baadhi ya wabia wanafanya uzalishaji bila kumshirikisha na bila kumpatia stahiki zake, huku upande mwingine ukieleza kuwa katika leseni hizo bado haujaanza uzalishaji.
Baada ya kusikiliza pande zote, Dkt. Kiruswa amewataka wamiliki hao kuweka mfumo wa wazi na wa pamoja wa mawasiliano, huku wakihakikisha kila mmoja anatambua mipaka na maeneo ya leseni wanazomiliki ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kusababisha migogoro.
Aidha, amewataka wachimbaji wadogo kujenga utamaduni wa kuaminiana, kushirikiana na kuheshimiana, akisisitiza kuwa chuki na kutokuelewana miongoni mwa wabia kunaweza kuchelewesha maendeleo na kupunguza manufaa yanayopaswa kupatikana kutokana na rasilimali madini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ametoa angalizo kwa wamiliki wa leseni nchini kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni walizopewa na Serikali, akieleza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa leseni ambazo hazijaendelezwa kwa mujibu wa masharti yake.
Amesema leseni ambazo zitabainika kutotumika kwa shughuli za uchimbaji kwa mujibu wa taratibu zitafutwa na maeneo hayo kutolewa kwa wachimbaji wenye uwezo na nia ya kuendeleza shughuli za uchimbaji.
Dkt. Kiruswa amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo ili waweze kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini na kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa pia ametembelea na kukagua shughuli za Soko la Madini la Mkoa wa Mwanza, akijionea namna shughuli za biashara ya madini zinavyoendeshwa na kusisitiza umuhimu wa masoko hayo katika kuwawezesha wachimbaji kupata soko rasmi na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

