Meneja wa mfuko WA Taifa wa BIMA ya Afya(NHIF)Mkoani Ruvuma Hance John wa pili kulia,akiwa katika Picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya Mantra
……….
Na Mwandishi wetu, Songea
KAMPUNI y MANTRA Tanzania Ltd inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya urani katika mto Mjini wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imetumi zaidi ya shilingi milioni 50 kugharimia Bima ya Afya kwa wote kwa wanafunzi 1,000 wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uwajibikaji kwa jamii.
Afisa Mahusiano wa MANTRA Tanzania Ltd, Yahanis Kilave, alisema,kampuni hiyo ina vipaumbele mbalimbali katika kusaidia jamii, ambavyo ni afya, maji, elimu, michezo na vinginevyo.
Alisema,wameona umuhimu wa kushirikiana na NHIF kuhakikisha wanafunzi hao wanapata uhakika wa huduma za afya ili waweze kushiriki katika masomo yao vizuri.
Kilave alisema, MANTRA Tanzania Ltd inaamini kuwa baada ya wanafunzi hao kupata bima za afya wataweza kuzingatia masomo, kufanya vizuri na baadaye kuwa sehemu ya watu ambao kampuni itawahitaji.
“Tuna imani baada ya kutoa bima hizi watazingatia masomo yao watafanya vizuri ili tupate watu tutakaowahitaji baadaye,” amesema Kilave.
Amewashukuru watumishi wa NHIF hasa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Meneja wa Mkoa wa Ruvuma Hans John kwa kazi kubwa waliyoifanya, akisema wanaamini bima hizo zitawasaidia vijana kuzingatia elimu na kufanikiwa katika maisha yao.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Ruvuma Hansi John alisema, mfuko huo una dhamana kwa wana Ruvuma na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa matibabu.
Alisema NHIF ina jukumu la kuwafikia watumishi wa umma, sekta binafsi pamoja na makundi makubwa ya wakulima kupitia AMCOS zao, wakiwemo wakulima wa kahawa, tumbaku na mahindi, huku watoto wakiwemo wanafunzi wakifikiwa kupitia Bima ya Toto ambayo gharama yake kwa mwaka ni shilingi 50,400.
Alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan,inalenga kuona kila Mtanzania anapata matibabu kwa kutumia bima ya afya na siyo fedha taslimu, kwa kuwa maradhi hutokea bila taarifa.
Ameishukuru MANTRA Tanzania Ltd kwa kufadhili bima hizo kwa wanafunzi 1,000 na kuzitaka kampuni nyingine kuiga mfano huo kwa kusaidia jamii na kurudisha kwa jamii kile wanachozalisha.
“kuwasaidia watoto kupata bima ya afya ni jambo muhimu kwa sababu mtoto anapokuwa na uhakika wa matibabu huondolewa hofu, hujawa na ujasiri na kujiamini, jambo linaloweza kumsaidia katika masomo na maisha yake kwa ujumla”alisema.
Katika tukio hilo, NHIF Mkoa wa Ruvuma imekabidhi cheti cha utambuzi kwa MANTRA Tanzania Ltd kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo kwa jamii, ikiwemo uwezeshaji wa bima za afya kwa wanafunzi 1,000.
John amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha Watanzania wanafikiwa na huduma za NHIF, hususan katika utekelezaji wa mpango wa Serikali wa Bima ya Afya kwa Wote.
