Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limesema kwa nyakati tofauti, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa saba wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa uhalifu unaohusisha matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji na wizi wa pikipiki.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Justine Masejo amesema miongoni mwa waliokamatwa yupo mwanamke mmoja anayedaiwa kutumika kama abiria kukodi bodaboda na kuwaelekeza madereva kwenye maeneo ambako wahalifu wenzake walikuwa wakisubiri kwa ajili ya kutekeleza matukio ya uhalifu.
Amesema uchunguzi wao umebaini kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu, ikiwemo baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni, na tayari wamewafikisha mahakamani na mashauri yao yapo katika hatua mbalimbali za kisheria.
Ameendelea kufafanua kuwa miongoni mwa matukio hayo ni tukio la mauaji ya Anold Osward (28) mkazi Orolesho, kata ya Olasiti Jijini Arusha yaliyotokea Juni 19, 2026 huko katika Mtaa wa Olteves, kata ya Olmot Jijini Arusha ambapo baada ya mahojiano ya kina watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika tukio hilo na matukio mengine katika wilaya ya Arumeru.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani humo limesema linaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la mauaji ya Hamis Idd Masimba (22) dereva wa bodaboda na mkazi wa Olasiti Jijini Arusha.
Kamanda Masejo amesema marehemu anadaiwa alipotea tangu Septemba 09, 2026, baada ya kumchukua abiria, na mwili wake ulipatikana Septemba 12, 2026 ndani ya nyumba ambayo haijakamilika, iliyopo katika maeneo ya Stendi Mpya, Mtaa wa Bondeni City jijini Arusha.
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Sambamba na hilo, limewasihi waendesha bodaboda na wamiliki wa pikipiki kuwa makini wanapobeba abiria au kukodisha pikipiki zao kwa ajili ya safari, hususani nyakati za usiku, kuhakikisha wanatoa taarifa mapema pindi wanapobaini mwenendo wowote wa kutia shaka.

