Na Mwandishi wetu, Kiteto

BAADHI ya wakazi wa kijiji cha Loltepes kata ya Sunya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, wamempokea mbunge wao Edward Ole Lekaita kwa mtindo wa aina yake kwa kupanda juu ya miti ili kumuona.

Ole Lekaita akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye kijiji cha Loltepes amewashukuru wananchi hao kwa upendo mkubwa waliouonyesha kwake.

Amesema mara baada ya kutoka Bungeni jijini Dodoma kuwazungumzia wana Kiteto, sasa ni muda wa kuwatembelea, kuwasikiliza na kuwapa mrejesho.

“Matarajio yetu ni kuiona Kiteto mpya ya maendeleo yenye shule za sekondari kila kata, huduma za afya maji na miundombinu ya barabara zinazopitika kila msimu,” amesema Ole Lekaita.

Amesema ana deni kubwa na wana Kiteto kwani wamempa heshima kubwa kwa kumchagua kwa kura nyingi hivyo atawatumikia kwa nguvu zake zote.

“Nitaendelea kuwa sauti ya wana Kiteto kwa kuwasemea na kuwatetea kila mahali husika kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya eneo hili,” amesema Ole Lekaita.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Athumani Kilimo (Msimbazi) ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sunya, amempongeza Ole Lekaita kwa namna anavyowapambania wana Kiteto.

“Mbunge wetu anapambana kuisemea Kiteto ili ipate maendeleo kupitia miradi ya maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara,” amesema Msimbazi.