Na Mwandishi wetu, Kigoma 
Hatua ya Serikali ya kuendelea kuboresha utoaji huduma za ardhi kwa njia za kidijitali imezidi kuimarika baada ya mfumo wa e-Ardhi kutua mkoani Kigoma, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Wataalamu wa ardhi kutoka halmashauri za Kasulu Mjini, Kigoma-Ujiji, Uvinza na Kibondo, wanaoshiriki mafunzo ya mfumo huo, wamepokea kwa shangwe ujio wa e-Ardhi, wakieleza kuwa utasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na kasi katika utoaji wa huduma.
Akizungumza kuhusu mfumo huo, Afisa Mipango Miji Mwandamizi kutoka Halmashauri ya Kasulu Mjini, Bw. Saimon Mahondo, amesema, matumizi ya e-Ardhi yatapunguza ulazima wa wananchi kusafiri umbali mrefu kwenda katika ofisi za ardhi kufuatilia huduma.
Kwa upande wake, Bi. Asia Mohammed, ambaye ni miongoni mwa wataalamu wanaoshiriki mafunzo hayo, amesema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za ardhi kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.
Wataalamu hao wameeleza kuwa, kupitia e-Ardhi, baadhi ya huduma ambazo awali zilihitaji mwananchi kufika moja kwa moja katika ofisi za ardhi, sasa zinaweza kuanzishwa au kufuatiliwa kwa njia ya mtandao.
“e-Ardhi inakwenda kumleta mwananchi karibu na huduma. Badala ya kusafiri kwenda ofisini kufuatilia huduma, sasa teknolojia inamwezesha kuanza mchakato akiwa alipo,” wameeleza wataalamu hao.
Aidha, wamesema matumizi ya mfumo huo yanatarajiwa kupunguza muda na gharama ambazo wananchi wamekuwa wakitumia kufuatilia huduma za ardhi, huku yakiboresha uwazi na ufanisi wa utoaji wa huduma.
Mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu hao ni sehemu ya maandalizi ya kuwawezesha kuwa na uelewa na uwezo wa kutumia mfumo wa e-Ardhi, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati katika maeneo yao.