Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (wa pili kulia), wakisikiliza maelezo ya taaluma inayotolewa na Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA, walipotembelea moja ya sehemu ya Chuo hicho inayohusika na utoaji mafunzo ya utengenezaji wa roboti kwa ajili ya matumizi mbalimbali, jijini Seoul, nchini Korea Kusini. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Noel Kaganda (katikati), Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade (wa pili kushoto) na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedeck Mbise (wa tatu kushoto nyuma).

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (katikati), Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Noel Kaganda (kulia) na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedeck Mbise (nyuma), wakiangalia moja ya roboti inayotengenezwa na Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA, wakati walipotembelea chuo hicho jijini Seoul, nchini Korea Kusini, pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika, KOAFEC.


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa pili kushoto), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (wa pili kulia), Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Noel Kaganda (kushoto) na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade (kulia) wakiangalia moja ya roboti inayotengenezwa na Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA, wakati walipotembelea chuo hicho jijini Seoul, nchini Korea Kusini, pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika, KOAFEC. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Seoul, nchini Korea Kusini)

Na Benny Mwaipaja, Seoul, Korea

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameongoza Ujumbe wa Tanzania kutembelea Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA, jijini Seoul nchini Korea Kusini, pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika, KOAFEC, akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb).

Mhe. Balozi Omar, alitoa hotuba fupi ya shukrani, na kusisitiza kuwa Tanzania imejipanga kuendeleza ushirikiano kati yake na Chuo hicho.

Aidha, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), kwa upande wake alisisitiza kuwa ziara yao katika Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA  ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kufuatia ziara za awali za viongozi wa Tanzania nchini humo.

Alieleza kuwa matumizi ya akili unde (AI) na mabadiliko ya kidijitali ambayo Chuo hicho imekuwa ikifundisha ni nguzo kuu za maendeleo ya Tanzania, na Serikali inalenga kuimarisha ujuzi wa vijana, miundombinu ya data, na mifumo ya uvumbuzi kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

Mhe. Kairuki alitoa mapendekezo tisa mahususi ya ushirikiano, yakilenga kuanzia utiaji saini wa MOU, kubadilishana wanafunzi, mafunzo ya wahadhiri, hadi kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Utafiti (Korea-Tanzania Digital Innovation Lab).

Alionesha imani yake kuwa ERICA ina uwezo wa kutekeleza mapendekezo hayo na alisisitiza umuhimu wa kuona matokeo ya haraka, kama vile mafunzo ya rasilimali watu, ujenzi wa maabara, na kuanzishwa kwa kampuni changa (startups).

Alihitimisha kwa kutoa mwaliko rasmi kwa Makamu wa Rais wa ERICA, Baek Dong-hyun, na ujumbe wake kutembelea Tanzania (Dodoma, Dar es Salaam, na Zanzibar) ili kuona fursa na utayari wa nchi katika kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji unaopatikana nchini katika sekta mbalimbali.

Katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Chuo hicho Prof.  Dong Baek, alijibu mapendekezo ya Mhe. Waziri Kairuki, akisema ni ya busara na muhimu.

Alikiri kuwa baadhi ya mapendekezo hayo yanaweza kutekelezwa kwa urahisi kwa sababu Serikali ya Korea tayari imetenga fedha kwa ajili ya ushirikiano na Tanzania, hivyo hakutakuwa na changamoto kubwa katika kuyaendesha.

Prof. Baek aliahidi kuwa Chuo kitayapitia mapendekezo hayo kwa kina ili kutafuta njia bora za kuyafanikisha.

Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA ni Chuo kinachozingatia sana utafiti na teknolojia, hasa katika nyanja za AI, data science, robotics, cybersecurity, na semiconductors, Kina mfano wa kipekee wa elimu unaoitwa ICPBL (Industry-Coupled Problem-Based Learning) na mifumo ya kisasa ya kujifunza kwa masafa na kinafanya kazi kwa karibu na viwanda na sekta ya teknolojia, kikiwa na miundombinu kama Campus Innovation Park na Ansan Science Valley.

Aidha, Chuo hicho kinafahamika kama mfano wa kimataifa wa jinsi elimu, utafiti, na viwanda vinavyoweza kukua pamoja, na kina uwezo wa kutoa mafunzo ya hali ya juu na kinafanya ushirikiano na vyuo vingine vya kimataifa.