Wananchi wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa katika kipindi kijacho kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu mwenendo wa hali ya hewa na uwezekano wa mvua za El Niño.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Rukia Zuberi ambapo amesema wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, yakiwemo mabondeni, maeneo ya jirani milima au mito, pamoja na maeneo yenye uwezekano wa kukumbwa na mafuriko au maporomoko ya ardhi, wanashauriwa kuchukua hatua tahadhari mapema, ikiwemo kuhama maeneo hayo, kuweka akiba ya chakula na mahitaji muhimu kwa matumizi wakati wa mvua hizo.

Pia amewahimiza wananchi kuhakikisha kuwa mitaro, mifereji na njia za maji zinakuwa safi na hazijazibwa na taka, ili kuwezesha maji kupita kwa urahisi hatua inayolenga kupunguza uwezekano wa maji kujaa katika maeneo ya makazi, kusababisha mafuriko na uharibifu wa mali na kuhatarisha maisha ya watu.

Kuhusu watoto, wazazi na walezi wametakiwa kuwa waangalifu na kutowaruhusu kwenda shuleni wakati mvua zinapokuwa kubwa na mazingira yakiwa hatarishi huk, viongozi katika maeneo mbalimbali wakielekezwa kusimamia utekelezaji wa tahadhari hizo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usafi wa njia za maji unafanyika kwa wakati.

TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha kuanzia mwishoni mwa Septemba 2026 na kuendelea hadi Januari 2027, Wananchi wa Mwanga wametakiwa kuendelea kufuatilia taarifa rasmi kutoka TMA na Serikali, pamoja na kuzingatia maelekezo yatakayotolewa ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.