Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Amos Pallangyo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 07, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali imewekeza jumla ya Shilingi bilioni 67.9 katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza Septemba 07,2026 Jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo, amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 27.8 zimetolewa kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), huku Wizara ya Fedha ikiwezesha taasisi hiyo kupata Shilingi bilioni 45.2 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya miundombinu.
Aidha,amebainisha kuwa uwekezaji huo umeenda sambamba na upanuzi wa TIA, ambapo idadi ya kampasi imeongezeka kutoka sita mwaka 2022 hadi kufikia nane, baada ya kuongezwa Kampasi za Zanzibar na Tanga. Kampasi hizo ni Dar es Salaam, Singida, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma, Zanzibar na Tanga.
Aidha amebainisha kuwa kupitia fedha hizo, miradi mbalimbali inaendelea katika kampasi za Singida, Mwanza, Kigoma, Zanzibar, Mbeya na Mtwara. Mradi wa jengo la taaluma Kampasi ya Singida umefikia asilimia 72, huku ujenzi wa mabweni mawili Kampasi ya Mwanza ukifikia asilimia 96.
Katika Kampasi ya Mwanza, jengo la taaluma na utawala limekamilika kwa asilimia 100 na limeongeza uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,620 kwa wakati mmoja, huku jengo la taaluma na utawala Kampasi ya Kigoma likifikia asilimia 98 na tayari linatumika. Kwa upande wa Mbeya, jengo la kumbi za mihadhara, maktaba na maabara ya kompyuta limekamilika kwa asilimia 100.
Katika eneo la wanafunzi, Prof. Pallangyo amesema idadi imeongezeka kutoka wanafunzi 24,494 mwaka 2022 hadi 37,397 mwaka huu wa taaluma, sawa na ongezeko la asilimia 52.7.
Ameongeza kuwa kati ya wanafunzi hao, 19,342 ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka HESLB, sawa na asilimia 51.7, huku wanafunzi 137 wa Kampasi ya Zanzibar wakinufaika na mikopo kutoka Zanzibar Higher Education Students’ Loan Board.
Aidha amebainisha kuwa TIA imeongeza programu za mafunzo kutoka 49 mwaka 2022 hadi 54, zikiwemo Shahada ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Shahada ya Uchumi na Fedha.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano, TIA imekuwa na wahitimu wapatao 62,680, huku taasisi hiyo ikiendelea kuimarisha uwezo wa watumishi ambapo kwa sasa ina maprofesa tisa. Watumishi 78 wamefadhiliwa kwa ajili ya masomo ya shahada za juu, kati yao 48 wamehitimu na 30 wanaendelea na masomo ya PhD.
Ameongeza kuwa TIA imepanua pia upatikanaji wa programu za shahada ya uzamili kutoka Kampasi ya Dar es Salaam pekee hadi Kampasi za Zanzibar, Mbeya na Singida, huku Kampasi ya Mwanza ikitoa fursa hiyo kuanzia mwaka huu.
