Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

 Jumla ya Sh milioni 4.5 zimetolewa na waumini wa Kanisa la Dar es Salaam Pentecostal Church (DPC) kutoka Kanda ya Kigamboni na Central Zone kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Msaada huo umehusisha fedha taslimu pamoja na mahitaji mbalimbali ya watoto ikiwemo wipes, sabuni za kufulia, maziwa, mafuta ya kujipaka na sabuni za kuogea, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwafariji watoto na wazazi wanaokaa hospitalini wakati wa kuwauguza.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya alisema msaada huo ni wa muhimu kwani watoto hao hutoka katika maeneo mbalimbali nchini na baadhi yao hukaa hospitalini kwa muda mrefu.

“Wazazi na walezi wa hawa watoto hukaa hospitalini kwa muda mrefu na  kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji, tukipatq wadau kama hawa wanakuwa wamepata mahitaji yao muhimu”, alisema Mallya

Kwa upande wake Mchungaji kutoka Dar es Salaam Pentecostal Church (DPC) Martin Mwaisumo alisema hatua hiyo imetokana na dhamira ya kanisa kutekeleza mafundisho ya upendo kwa vitendo ambapo waumini kutoka jumuiya mbalimbali wameungana kutoa msaada kwa watoto hao.

“Tumekusanyika pamoja na tumeona ni vyema tuje kuonyesha upendo, Yesu alikuja duniani kuonyesha upendo hivyo sisi nasi tumeona ni muhimu kuonyesha upendo huo kwa vitendo”, alisema Mwaisumo.

Naye Kiongozi kutoka City Center Cell Pamela Deteba alisema maandalizi ya msaada huo yalihusisha ushiriki wa waumini mbalimbali waliotoa michango yao kwa lengo la kuhakikisha watoto na walezi wao wanapata mahitaji muhimu wanapokuwa hospitalini.

“Yote haya ni kwa ajili ya moyo wa upendo wa kusherehekea na wale ambao ni wahitaji. Mungu awabariki sana watu wa JKCI kwa kutufungulia milango na kuturuhusu kutoa msaada huu”, alisema Deteba

“Tunawapongeza sana madaktari wauguzi na wafanyakazi wote wa JKCI kwa kazi nzuri mnayoifanya kuhakikisha kwamba watoto hawa wanakuwa na afya njema, kazi hii si rahisi Mungu awabariki sana.” alisema Deteba

Msaada huo ni sehemu ya ushirikiano kati ya JKCI na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa hususanI watoto wanaohitaji matibabu ya moyo ambao wakati mwingine hulazimika kukaa hospitalini kwa muda mrefu.