Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Bw. Charles Kadonya amefungua Kikao cha Kamati ya Maandalizi ya Zoezi la Utoaji Elimu kwa Umma kuhusu rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki, katika hafla iliyofanyika leo tarehe 07 Septemba, 2026 mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bwana Kadonya amesema kikao hicho kinalenga kuweka mikakati na utaratibu wa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu mchakato huo kabla ya kutoa maoni yao.
Alisema maandalizi hayo yanahusisha kupanga mkakati wa utoaji elimu kwa umma, kubaini mikoa itakayotembelewa, kuandaa mbinu bora za kuwafikia wananchi pamoja na kuandaa bajeti ya zoezi hilo.
Bwana Kadonya amebainisha kuwa Fungamano la Kisiasa likifanikiwa litaiwezesha jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarisha nguvu za pamoja za nchi wanachama katika maeneo ya uchumi, biashara, usalama na utoaji wa huduma za jamii.
Amesema hatua hiyo pia itafungua fursa mpya za maendeleo, kuwaunganisha wananchi wa nchi wanachama na kuimarisha nafasi ya Jumuiya katika majukwaa ya kimataifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni kuhusu Fungamano la Kisiasa. Amesema wananchi wanapaswa kushirikishwa kwa haki na kupewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu mchakato huo, ili kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia maslahi na mitazamo ya wananchi wa Jumuiya.
“Uwepo wetu hapa Morogoro kwa siku hizi tano ni uthibitisho kwamba tunayo dhamira thabiti ya pamoja ya kufanikisha mchakato huu kwa weledi na uwazi ili kufikia malengo yanayotarajiwa,” alisema Bw. Kadonya
Zoezi hilo kwa upande wa Tanzania litafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha utoaji elimu kwa umma na awamu ya pili itakuwa ni ukusanyaji wa maoni ya wananchi kupitia Timu ya Wataalam ya Uandishi wa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki, ambao watakutana na wadau katika mikoa itakayobainishwa ili kupata maoni yatakayosaidia katika mchakato wa uandaaji wa Rasimu ya Katiba hiyo.
Bwana Kadonya ameongeza kuwa Uanzishwaji wa EAC uliweka hatua nne za mtangamano wa kikanda ambazo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.

