************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
WATUMISHI Saba wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) wanashikiliwa na Jeshi la polisi mkoani Pwani, wakidaiwa kuiba raslimali vifaa vyenye thamani ya sh.mil.15 ambavyo walikuwa wakivichepusha ,kisha kuuza kwa maslahi yao binafsi.
Kati ya watumishi hao walipopekuliwa kwenye makazi yao ,pia walikutwa na vitambulisho vya Taifa boksi moja ambalo ndani vimo vitambulisho 15,000 pamoja na komputa mpakato mbili na nyaya za komputa.
Akielezea juu ya tukio hilo ,kamanda wa polisi mkoani Pwani (ACP) Wankyo Nyigesa alisema ,kati ya watuhumiwa hao wanaodaiwa kufanya tuhuma hizo sita ni wanaume na mmoja mwanamke ambapo majina yao yanehifadhiwa kwa uchunguzi zaidi.
Hata hivyo,kamanda huyo alibainisha,taarifa za tukio hilo zilipokelewa kutoka kwa uongozi wa juu wa NIDA kwenda jeshi la polisi mkoa Juni 14 mwaka huu na mara moja lilifuatilia na kuwakamata watuhumiwa saba na gari T.365 DFS aina ya Toyota spacio rangi ya silver ambayo ilikuwa imebeba jenereta moja mali ya NIDA.
“Awali watumishi wa NIDA waliokuwa wanafanya kazi mkoani hapo walikuwa wanatumia ofisi za kilipokuwa kiwanda cha kubangua korosho TANITA KwaMatias Kibaha na baadae serikali iliwajengea ofisi mpya za kisasa eneo la Machinjioni huko Loliondo Mjini Kibaha.”
“:Baaada ya majengo kukamilika walitakiwa kuhamia katika ofisi hizo mpya wao wenyewe na vitendea kazi vyao kama komputa,meza,scanner,camera,stationaries,BVR kits na vingine”alifafanua Wankyo.
Wankyo alielezea,watumishi wanaoshikiliwa na polisi waliteuliwa na uongozi wa mamlaka hiyo kuhamisha raslimali vifaa kutoka TANITA kwenda Loliondo ambapo wakiwa njiani walikosa uaminifu na kuanza kuvichepusha ,kuviuza na kujipatia pesa kwa manufaa yao binafsi .
Wankyo alitoa rai kwa watumishi wa umma , taasisi na mashirika ya watu binafsi wanapokabidhiwa madaraka na mali za serikali wawe waaminifu ,watiifu kwa kuzilinda kama mboni ya jicho lao na amekemea kuacha ubadhilifu wa mali za umma kwa maslahi ya matumbo yao.