Home Mchanganyiko WIZARA YAWAKUMBUKA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM BUHANGIJA

WIZARA YAWAKUMBUKA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM BUHANGIJA

0

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Mwajuma Magwiza akikagua moja ya bweni lililopo katika Shule ya Msingi ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum ya Buhangija wakati alipotembeela shule hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Mwajuma Magwiza akizungumza na wanafunzi wa Shule Msingi ya wenye mahitaji maalum Buhangija(hawapo pichani) wakati alipoitembelea shule hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Mwajuma Magwiza (kulia) akimkabidhi fedha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buhangija Bw. Seleman Kipanya(kushoto) kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi waliobaki shuleni hapa katika kipindi hiki cha likizo

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Mwajuma Magwiza akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Bwangija, walimu, wafanyakazi na Maafisa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

*************************

 Na Mwandishi Wetu Shinyanga

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto   ( Idara Kuu Maendeleo ya Jamii) imewatembeea watoto wanaosoma katika shule ya Msingi Buhangija iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga ikiwa ni kuadhimisha Siku ya Mtoto wa  Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Bi. Mwajuma Magiwza amesema Wizara kama msimamizi wa Sera ya Mtoto na Sheria ya Mtoto ina jukumu la kuhakikisha Taasisi zote zinaoshughulika na masuala ya mtoto zinahakikisha zinawalinda, zinawatunza na kuwandeleza watoto.

Ameongeza kuwa Shule hiyo ilianzishwa kwa madhumuni dhabiti ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalum kupata huduma ya Elimu na huduma zao zingine kwa urahisi ndio maana  wameanzisha shule ya Msingi yenye bweni.

Bi. Magwiza amesema kuwa ingawa shule hiyo iko chini ya Manispaa ya Shinyanga lakini kama Wizara inawajibika pia katika kutatua changamoto za Shule hiyo ikiwemo upatikanaji wa huduma za Afya kwa watoto na wataalam watakaowasaidia watoto hao kupata elimu katika mazingira salama.

“Si jukumu la Serikali tu kuhakikisha changamoto za Shule kama hizi zinatatulika ila pia na wananchi na wadau mbalimbali tuunge mkono juhudi za Serikali katika kusaidia kutatua changamoto hizo na sio kwa shule hii tu hata kwa nyingine” Alisema

Akitoa taarifa kuhusu Shule ya Msingi ya Buhangija  Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw. Selemani Kipanya amesema kuwa kuwa Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 230 wakiwemo watoto wenye ualbino 134 ikiwa savula 70 na wasichana 64, watoto viziwi 73 ikiwa wavulana 37 na wasichana 36 huku watoto wasiiona ni 23 wavulana 13 na wasichana 10.

Bw. Kipanya amesema kuwa changamoto kubwa zinazoikabili Shule hiyo ni kwa baadhi ya wazazi kushindwa kuwafuata watoto wao wakati wa likizo na hivyo kuendelea kuwalea kwa muda wote wa likizo, uhaba wa mafuta maalum kwa ajili ya watoto wenye ualbino na watoto wengi kutokuwa na Bima ya afya CHf kwa ajili ya kupata matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Geofrey Mwangulumbi akizungumza na ujumbe huo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amewashukuru kwa kuja kitembelea  shule hiyo na kusema kuwa ni jambo jema na litaleta mwanga na  muamko kwa Taasisi nyingine za Serikali na wadau wengine kuja kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Naye mmoja wa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Buhangija Nchambi Kashindye ameishukuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuwakumbuka kwa kuwaletea zawadi mbalimbali ambazo zitawasaidia katika kipindi cha likizo kwa wale walioko shuleni.

Shule ya Msingi Buhangija iliyopo Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyana ni shule ya msingi iliyojengwa na kutengwa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo watoto viziwi, wasioona na wenye ualbino.