Katibu Tawala wa wilaya ya Mbinga Pendo Daniel Ndumbaro,akitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga,katikati Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Joseph Kashushura na kushoto Mwenyekiti wa Halmashauri Desderius Haule
Na Mwandishi Wetu,Mbinga
KATIBU Tawala Wilaya ya Mbinga Pendo Daniel Ndumbaro, amewataka madiwani wa Halmashauri ya wilaya Mbinga,kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata kwenye maeneo yao kupandisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari kwakuwa elimu ndiyo msingi mkuu wa maendeleo.
Ndumbaro,ametoa wito huo wakati alitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne kwa mwaka wa 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri wilaya kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga.
” Mbinga DC tuko vizuri kwenye maeneo mengine ya maendeleo kuliko halmashauri nyingine nane za mkoa wa Ruvuma,lakini kwenye elimu bado zianahitaji juhudi kubwa za pamoja ili kuongeza ufaulu. kwa vijana wetu”alisema Ndumbaro
Ndumbaro ameeleza kuwa, Halmashauri tayari imeonyesha jitihada kubwa za makusudi kwa kufanya ziara na kutembelea shule kwa ajili ya kukagua mazingira ya ujifunzaji,ufundishaji na kufuatilia maendeleo ya taaluma.
Amebainisha kuwa, ushirikiano wa karibu kutoka kwa madiwani katika ngazi za kata utaongeza chachu ya kuleta matokeo bora zaidi kwenye mitihani ya kitaifa.
Katika hatua nyingine, Pendo Ndumbaro, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji pamoja na timu yake ya wataalamu kwa kazi kubwa iliyotukuka ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambapo Halmashauri imefanikiwa kuvuka lengo na kufikia asilimia 120 huku akisisitiza juhudi ziongezwe katika kubuni vyanzo vipya vya mapato ikizingatiwa kuwa Halmashauri hiyo imeongezewa makisio ya makusanyo hadi kufikia bilioni 14 mwaka 2026/2027.
Pamoja na mafanikio hayo ya kifedha,amepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa katika kutatua kero za miundombinu ya barabara kwa kuzichonga na kuziweka katika hali inayopitika kwa urahisi muda wote,ili kurahisisha usafirisha wa wananchi,usafirishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali za kijamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Desderius Haule,ametaka kuharakishwa kwa utekelezaji wa uwekezaji katika maeneo yote yanayomilikiwa na halmashauri hiyo kwa kujenga miradi ya kimkakati itakayoongeza mapato.
Aidha amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseph Kashshura, kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ili kushughulikia upatikanaji wa vibali vinavyohitajika Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo iki uanze haraka kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi hiyo ipo ndani ya eneo la Halmashauri ya Mbinga Mji, jambo linalotoa fursa kubwa ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Haule,uwekezaji ukifanyika katika maeneo hayo Halmashauri ya Mji nayo itanufaika kwa kiasi kikubwa kupitia ushuru wa majengo pamoja na kodi nyingine za kisheria.
“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania anasisitiza kila Halmashauri iwe na uwekezaji ili kuongeza mapato. Mbinga DC tunataka miradi ya kimkakati itakayoiletea Halmashauri yetu faida.” alisisitiza Haule.
Aliwataka Madiwani kurejea kwenye Kata zao na kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe wa kamati zote za Baraza la Madiwani kwa ushirikiano mzuri waliouonyesha pamoja na Menejimenti ya Halmashauri katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, hatua iliyofanikisha utekelezaji wa majukumu ya halmashauri kwa ufanisi.
