Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media

Serikali wilayani Same imesisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wenye umri chini ya miaka 10 wanapatiwa chanjo ya Polio ya matone, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo hatari. Aidha, wananchi wametakiwa kutosikiliza taarifa zinazopotosha kuhusu usalama wa chanjo, bali kuzingatia elimu na maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Same, Bi. Mamndolwa Gembe, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya Polio Awamu ya Kwanza kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10 wilayani humo.

Bi. Mamndolwa amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha watoto wanakuwa salama na wenye afya njema kupitia huduma mbalimbali za afya, ikiwemo chanjo ya Polio, ambayo ni miongoni mwa hatua muhimu za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Amesema ugonjwa wa Polio ni hatari kwa kuwa hushambulia mfumo wa fahamu na unaweza kusababisha kupooza kwa mwili, ulemavu wa kudumu na hata kifo. Hivyo, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wenye umri chini ya miaka 10 wanapata chanjo hiyo, akisisitiza kuwa chanjo ya Polio ni salama na ina umuhimu mkubwa katika kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huo.

“Ugonjwa wa Polio ni hatari sana kwani unashambulia mfumo wa fahamu na unaweza kusababisha kupooza kwa mwili na hata kifo. Tuhakikishe watoto wetu wenye umri chini ya miaka 10 wanapata chanjo hii ya Polio, kwa sababu chanjo hii ni salama,” amesema Bi. Mamndolwa.

Aidha, amewataka wahudumu wa afya, watendaji wa Serikali, wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na walimu kuongeza juhudi za kutoa elimu na hamasa kwa wananchi katika maeneo yote ili kuhakikisha jamii inapata uelewa sahihi kuhusu umuhimu wa chanjo.

Amesema ushirikiano wa wadau hao ni muhimu katika kuhakikisha wazazi na walezi wanapata taarifa sahihi na kuwapeleka watoto wao kupata chanjo kwa wakati, hatua ambayo itasaidia kuwalinda dhidi ya ugonjwa wa Polio.

Kampeni ya Chanjo ya Polio Awamu ya Kwanza inafanyika katika mikoa minane nchini Tanzania kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026, ikiwa na lengo la kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huo kufuatia milipuko iliyotokea katika nchi jirani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampeni hiyo inawalenga watoto wote wenye umri chini ya miaka 10, huku Wilaya ya Same ikitarajia kuwafikia jumla ya watoto 85,677 kwa ajili ya kupata chanjo hiyo.