Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam

WANACHAMA wa Wadau Madale SACCOS wameanza mchakato wa kupata viongozi wa taasisi hiyo, huku wakitakiwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uzoefu katika uongozi, usimamizi wa fedha na kuwa na maono ya kuendeleza SACCOS hiyo.

Akizungumza katika kikao cha Wadau Madale Group kilichofanyika Kwa Magaigwa, Madale, Katibu wa Wadau Madale Group, Issa Mnasha, amesema mchakato huo unalenga kuhakikisha wanapatikana viongozi wenye uwezo wa kusimamia SACCOS kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa wanachama.

Mnasha amesema waombaji wa nafasi za uongozi wanapaswa kujaza fomu kwa usahihi na kutoa taarifa zinazohitajika, ikiwemo kueleza uzoefu wao katika uongozi na usimamizi wa taasisi za fedha, benki, vikundi vya kifedha, SACCOS au vikoba.

Amesema waombaji pia wanatakiwa kueleza uzoefu wao katika chama cha ushirika, ikiwemo muda ambao wamekuwa wanachama na mikutano ya vyama vya ushirika waliyowahi kuhudhuria, pamoja na manufaa wanayoamini yanaweza kupatikana kwa wanachama kupitia SACCOS hiyo.

Kwa mujibu wa Mnasha, kila mwombaji anatakiwa kuwa na maono ya wazi kuhusu anachotarajia kukifanya endapo atachaguliwa kuwa kiongozi, akisisitiza kuwa uongozi mzuri hauishii katika kutafuta nafasi, bali unahitaji kuwa na dira ya kuiendeleza taasisi.

Amesema viongozi wanaotarajiwa kuchaguliwa wanapaswa kueleza mambo muhimu wanayokusudia kuyatekeleza katika kipindi chao cha uongozi ili kuhakikisha SACCOS inakua na kufikia malengo yaliyowekwa na wanachama.

Aidha, Mnasha amesema waombaji wanapaswa kuweka wazi nafasi nyingine za uongozi walizonazo, ikiwemo nafasi za kisiasa au za serikali, na kueleza iwapo waliteuliwa au walichaguliwa na mamlaka husika.

Amesema kuwa kuwa na nafasi nyingine ya uongozi hakumzuii mwanachama kuomba uongozi katika SACCOS, isipokuwa ni muhimu wanachama wengine kufahamu nafasi hizo ili kuwepo uwazi katika mchakato wa uchaguzi.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa SACCOS hiyo, Mnasha amesema wanachama wameonyesha dhamira kubwa kwa kuchangia fedha na kuwezesha mchakato huo kuendelea.

Amesema kabla ya kusajiliwa kwa SACCOS hiyo, wanachama walikuwa tayari wamekusanya kiasi cha fedha kinachokaribia Sh milioni tatu, ambacho amesema ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha awali kilichohitajika kuonyesha utayari wa wanachama kuanzisha taasisi hiyo.

Amesema baada ya SACCOS kusajiliwa, wanachama wataendelea kufuata taratibu zote za msingi ikiwemo michango ya kila mwezi na masharti mengine yatakayoainishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za vyama vya ushirika.

Mnasha amesisitiza kuwa uongozi wa SACCOS unatokana na wanachama wake, hivyo hakuna mtu ambaye si mwanachama anayeweza kutoka nje na kuja kuwaongoza wanachama wa SACCOS hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wadau Madale SACCOS, amesema wanachama wamejitahidi kusimamia na kulinda fedha walizoweka katika benki, hatua ambayo imewezesha juhudi za kuanzisha SACCOS hiyo kuendelea.

Amesema sasa wanachama wanapaswa kukamilisha mchakato wa kujaza fomu na kupata viongozi watakaosimamia SACCOS hiyo ili ianze kutekeleza shughuli zake kwa manufaa ya wanachama.

Mwenyekiti huyo amewataka wanachama kutumia fomu zilizotolewa kwa ajili ya mchakato huo, akisema zimeandikwa kwa Kiswahili na zinaelekeza taarifa zinazopaswa kujazwa na kila mwombaji.

Amesema wanachama wana nafasi ya kutoa maoni na ushauri katika mchakato huo ili kuhakikisha uchaguzi wa viongozi unakamilika kwa wakati na SACCOS inaanza kazi rasmi.

Wadau Madale SACCOS inatarajiwa kupata viongozi wake kupitia mchakato unaoshirikisha wanachama, huku wanachama wakisisitizwa kuchagua viongozi wenye uwezo, uadilifu na maono ya kukuza taasisi hiyo.