Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Agosti 14, 2026
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amewasihi wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, akisema michezo ni muhimu katika kujenga afya na kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Ndemanga alitoa kauli hiyo wakati wa Baobab Marathon, iliyofanyika ikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Taasisi ya Baobab, huku tukio hilo likihusisha mbio za kilomita tano na 10 pamoja na michezo ya mpira wa miguu na kikapu.
Ndemanga alisema ushiriki wa wananchi katika michezo haupaswi kuishia kwenye mashindano pekee, bali unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa kuzingatia faida zake kiafya.
Mkurugenzi wa Baobab, Shani Swai, alielezea marathon hiyo imefanikiwa ,watu wamejitokeza pamoja na shughuli nyingine za maadhimisho ya miaka 20, ikiwa na malengo mawili ya kuhamasisha jamii kushiriki michezo na kuchangia shughuli za kijamii.
Kwa mujibu wa Shani, washiriki wameshindana katika mbio za kilomita tano na 10, mpira wa miguu na kikapu, huku waliofanya vizuri wakikabidhiwa tuzo.
Kwa upande wake, Muasisi wa Baobab, Sophia Mawenya, alifafanua Baobab Marathon siyo tukio la michezo pekee, bali ni sehemu ya jitihada za kutumia michezo kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za kijamii, hususan maendeleo ya kituo hicho.
Maadhimisho hayo yanafikia kilele Agosti 15, ambapo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, akishirikiana na viongozi, wazazi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu na maendeleo.
Taasisi ya Baobab ilianzishwa rasmi mwaka 2005 .

