Mratibu Msaidizi wa Idara ya Hesabu na Mhadhiri wa UDSM, Dkt. Sylivesta Rugeiyhamu akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. William Anangisye akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.

Happy Lazaro,Arusha 

ARUSHA. Wataalamu wa hisabati kutoka Afrika na nchi mbalimbali duniani wamekutana jijini Arusha katika mkutano wa pili unaolenga kuimarisha taaluma hiyo, utafiti na ufundishaji wake kwa ajili ya kuchochea maendeleo endelevu.

Mkutano huo umewakutanisha wataalamu kutoka zaidi ya nchi 30, zikiwemo Tanzania, Japan, Sweden na Norway, kwa lengo la kubadilishana uzoefu, maarifa na matokeo ya tafiti pamoja na kujadili namna ya kuendeleza matumizi ya hisabati katika kutatua changamoto za maendeleo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mgeni Rasmi ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. William Anangisye, amesema mkutano huo ni fursa muhimu ya kuimarisha ufundishaji wa hisabati kwa wanafunzi wa ngazi ya uzamili, sambamba na kukuza tafiti katika taaluma hiyo.

Amesema ushirikiano baina ya wataalamu hao unapaswa kuendelea kuimarishwa kupitia tafiti shirikishi na miradi mbalimbali inayohusiana na hisabati, hatua ambayo itasaidia kuongeza ufanisi katika ufundishaji na matumizi ya taaluma hiyo kwa maendeleo ya taifa.

“Hatua hii inatupa nafasi ya kuweka msisitizo wa somo la hesabu, kupewa kipaumbele kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu. Msingi mzuri wa hesabu kwa wanafunzi ni muhimu katika kuwaandaa kwa taaluma mbalimbali zinazohitaji ujuzi wa kihisabati,” amesema Prof. Anangisye.

Prof. Anangisye ameongeza kuwa hisabati ni taaluma inayopaswa kupewa kipaumbele kutokana na mchango wake katika maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini, akieleza kuwa taaluma hiyo ina nafasi kubwa katika kuzalisha walimu, wataalamu wa fedha, wachumi na wanasayansi.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Idara ya Hesabu na Mhadhiri wa UDSM, Dkt. Sylivesta Rugeiyhamu, amesema mkutano huo umeleta pamoja wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha utafiti shirikishi katika hisabati na elimu ya hisabati ili kuchochea maendeleo endelevu.

Amesema mkutano huo pia unalenga kuchambua kwa kina nafasi ya hisabati katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo, huku washiriki wakipata fursa ya kubadilishana uzoefu, maarifa na matokeo ya tafiti zinazohusiana na taaluma hiyo.

Dkt. Rugeiyhamu amesema miongoni mwa maeneo yanayojadiliwa ni matawi mbalimbali ya hisabati yanayohusiana na sayansi na teknolojia, pamoja na matumizi ya akili mnemba (AI), ambayo kwa sasa yanaendelea kuwa sehemu muhimu katika maendeleo ya taaluma na sekta mbalimbali.

Amesema ushiriki wa wataalamu kutoka zaidi ya nchi 30 unalenga kuhakikisha hisabati inapewa kipaumbele zaidi, inaendelezwa na kutumika kama nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya sayansi, teknolojia na maendeleo endelevu.