Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Waandishi wa Habari Agosti 13, 2026 jijini Dodoma kuhusu ufadhili wa masomo wa wanafunzi 10 kutoka Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) kilichopo jijini Moscow, nchini Urusi uliotolewa kupitia utaratibu wa Samia Scholarship Extended.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Jumla ya wanafunzi 10 waliomaliza kidato cha sita na kupata alama za juu katika tahasusi za PCM, PGM na PMC, wamepata ufadhili wa kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) kilichopo jijini Moscow, nchini Urusi.
Ufadhili huo umepatikana kufuatia ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo mnamo mwezi Juni, 2026 ambapo chuo hicho ndicho kilichomtunuku Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa).
Akizungumza na Waandishi wa Habari Agosti 13, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa wanafunzi hao wamepata ufadhili huo kupitia utaratibu wa Samia Scholarship Extended.
“Wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya kambi ya mafunzo nchini Urusi kwa takriban miezi 10, Serikali ya Urusi itagharamia mafunzo hayo kwa asilimia 80 na Serikali ya Tanzania itagharamia asilimia 20, watakapoanza mafunzo ya chuo kikuu mnamo Septemba 2027, Serikali ya Urusi itagharamia kwa asilimia 100”, amesema Prof. Mkenda.
Akifafanua juu ya upatikanaji wa wanafunzi hao, Mhe. Prof. Mkenda amesema kuwa wamechukua wale waliofaulu vizuri baada ya wale 50 wa mwanzo, hivyo wamechukua kuanzia mwanafunzi wa 51 hadi 60 ambapo kati yake, wanafunzi saba wametoka katika shule za serikali na wanafunzi watatu wametoka katika shule za binafsi.
Akizungumza kuhusu wanafunzi 50 waliochaguliwa hivi karibuni, amesema kuwa wote wamekubali kupokea ufadhili huo wa kusoma nje ya nchi na wanatarajia kuanza kambi ya mafunzo mnamo Septemba 14, 2026 kwa muda usiozidi miezi 10 katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela – Arusha (NM-AIST) kabla ya kwenda katika vyuo hivyo vya nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkenda ametoa rai kwa wanafunzi wanaopata ufadhili wa kusoma nje ya nchi kufanya vizuri kwenye masomo yao ili kuongeza ushawishi kwa nchi hizo kutoa ufadhili kwa wanafunzi wengine zaidi hali itakayosaidia mikopo ya elimu ya juu inayotolewa kwa wanafunzi nchini kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.

