Serikali wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, imemuokoa mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina limehifadhiwa, aliyekuwa ameachishwa shule na familia yake na kupelekwa kwa mwanaume kwa lengo la kumuozesha.

Mtoto huyo, mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Jiungeni, iliyopo Kata ya Ruvu wilayani Same, aliokolewa baada ya Serikali kupata taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu tukio hilo.

Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alisema baada ya kupokea taarifa hiyo alielekeza maafisa wa Serikali kufanya uchunguzi, ambapo walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 20 katika mazingira ya ndoa.

“Serikali inalaani vikali kitendo hiki cha kikatili cha kumnyima mtoto haki zake za msingi, ikiwemo haki ya kupata elimu na kukua katika mazingira salama,” alisema Kasilda.

Alisema watuhumiwa wamefikishwa mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya hatua za kisheria, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Serikali kuhusu vitendo vya aina hiyo.

Aidha, Kasilda alisema Shule ya Msingi Jiungeni ilijengwa mahususi kusaidia watoto kutoka jamii ya wafugaji wanaoishi katika eneo hilo kupata elimu.

Alisema kuna uwezekano wa kuwepo kwa wanafunzi wengine walioacha shule kutokana na ndoa za utotoni au kwenda kuchunga mifugo, hivyo Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu.

“Msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha watoto wanakwenda shule na sisi tutapambana na wazazi wanaokiuka maelekezo ya Serikali,” alisema.

Kasilda aliwapongeza maafisa wa Serikali pamoja na wananchi waliofanikisha zoezi la kumuokoa mtoto huyo, akisema walilazimika kufanya uchunguzi katika mazingira magumu ya porini ambako mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana huyo.

Pia aliwaonya watu wanaojaribu kutoa rushwa kwa lengo la kuwaachia watuhumiwa, akisema watakaobainika kufanya hivyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayehatarisha usalama, elimu na ustawi wa watoto.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema mtoto huyo atarejeshwa shuleni ili kuendelea na masomo yake.

Ndoa za utotoni zinaweza kuwanyima watoto fursa ya kupata elimu na kuwaweka katika mazingira hatarishi ya ukatili na unyanyasaji, pamoja na changamoto za kiafya na kisaikolojia.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa jamii kulinda haki za watoto, kuhakikisha wanapata elimu na kukua katika mazingira salama yanayozingatia maslahi na mustakabali wao.