Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeandaa mpango wa miaka mitano (2025/2026 hadi 2029/2030) wa kuendeleza miliki za Serikali (majengo/viwanja) vinavyomilikiwa na ofisi za Balozi duniani.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango huo Agosti 13, 2026 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Jumanne Maghembe alisema kuwa Serikali kupitia ofisi za Balozi inamiliki majengo 110 na viwanja 13 nje ya nchi.

Ameeleza kuwa mpango wa uendelezaji wa miliki hizo utatekelezwa kwa awamu kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali pamoja na vyanzo mbadala ikiwa ni pamoja na ubia na taasisi za fedha kama vile Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na benki. Mpango huo unalenga kuipunguzia Serikali gharama za kodi zinazotokana na kupangisha ofisi na makazi ya balozi na watumishi, kulinda na kuimarisha taswira ya nchi kimataifa. 

Mhe. Naibu Waziri Maghembe aliitaja miradi inayotekelezwa kwa bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 kuwa ni pamoja na ukarabati wa majengo katika ofisi za Balozi za Tanzania nchini Uswisi, Marekani, Uingereza, Nigeria, na Ethiopia. 

Miradi inayotekelezwa kwa kutumia vyanzo mbadala ambayo ina sura ya kitega uchumi ni pamoja na mradi wa majengo pacha ya ghorofa 22 Nairobi, Kenya na mradi wa jengo la ghorofa 25 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa upande wao, wajumbe wa NUU chini ya Mwenyekiti, Mhe. Najma Murtaza Giga waliipongeza Wizara kwa mpango huo na kusisitiza umuhimu wa kuusimamia ipasavyo ili ulete tija iliyokusudiwa.